Mwenendo wa upelelezi kesi ya Masamaki Februari 3

Aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Tiagi Masamaki.

Muktasari:

Hayo yameelezwa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Vitalis Peter mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, wa Mahakama ya Mkazi Kisutu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi  kwa kula njama na kuisababishia serikali  hasara ya Sh 12.7 bilioni inayomkabili aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Tiagi Masamaki na wenzake, utatoa taarifa za hatua za  upelelezi  ulipofikia Februari 3,2017.

Hayo yameelezwa leo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Vitalis Peter mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, wa Mahakama ya Mkazi Kisutu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo.

Mbali na Masamaki washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo  iliyotokana na sakata la makontena 329 ni Meneja Kitengo cha Huduma za Ushuru  TRA, Habib Mponezya  (45) na Meneja Msimamizi na Ufuatiliaji wa Forodha, Burton  Mponezya (51). 

Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha  ICD Azam, Eliachi  Mrema (31),  Mchambuzi  Mwandamizi  wa Masuala ya Biashara  TRA,  Hamis Omary (48), Meneja wa Oparesheni  za Usalama na Ulinzi  ICD, Raymond Adolf Louis (39) na Meneja wa Azam ICD, Ashrafu Khan (59) na Haroun Mpande (28) wa kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT TRA.

Kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Juni Mosi na Novemba 17, 2015 walikula njama kwa kuidanganya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Sh 12.7 bilioni.

Washtakiwa hao, wanadaiwa ku danganya kuwa Makontena 329 yaliyokuwepo katika Bandari Kavu ya Azam (AICD) yalitolewa baada ya kodi zote kufanyika wakati wakijua si kweli.