Mwijage aeleza siri viwanda kujengwa Pwani

Muktasari:

  • Mwijage alisema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha Kemikali cha Msufini kitakachojengwa Mlandizi, Pwani.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema ujenzi wa viwanda vingi mkoani Pwani ni jitihada za mkuu wa mkoa huo, Mhandisi Evarist Ndikilo.

Mwijage alisema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha Kemikali cha Msufini kitakachojengwa Mlandizi, Pwani.

Alisema sera ya viwanda inataka kujengwa viwanda nchi nzima lakini mkuu huyo wa mkoa anafanya jitihada kuhakikisha wawekezaji wanakwenda kwenye mkoa wake.

Mwijage alitoa ufafanuzi huo alipojibu hoja ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akisema viwanda vijengwe sehemu ambazo kuna rasilimali za kutosha na si Pwani pekee.

“Kama wawekezaji wa kiwanda cha nyanya wamekuja Pwani basi wapelekwe Iringa ambako nyanya zinalimwa kwa wingi, kama ni kiwanda cha maziwa basi waje kule kwetu Rungwe, tunazalisha maziwa mengi,” alisema Dk Tulia.

Hata hivyo, Mwijage alifafanua kwamba licha ya sera ya viwanda kutaka viwanda vijengwe kila mahali hapa nchini, mwitikio umekuwa mkubwa Pwani kwa sababu ya jitihada binafsi za Ndikilo.

“Wakati mwingine napenda kutofautiana, viwanda vingi vinajengwa Pwani kwa sababu ya Mkuu wa Mkoa,” alisema Mwijage kabla ya kuweka jiwe la msingi kwa niaba ya Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan.