Nani kuondoka na Sh1bilioni ya Mo Dewji

Muktasari:

Leo Oktoba 20, 2018 mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ amepatikana baada ya waliomteka kumtupa katika viwanja vya Gymkhana jijini hapa, lakini swali la kujiuliza ni nani atakayepata Sh1bilioni kwa kusaidia kupatikana kwa bilionea huyo


Dar es Salaam. Leo Oktoba 20, 2018 mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ amepatikana baada ya waliomteka kumtupa katika viwanja vya Gymkhana jijini hapa, lakini swali la kujiuliza ni nani atakayepata Sh1bilioni baada ya kusaidia kupatikana kwa bilionea huyo.

Mo Dewji alitekwa alfajiri ya Oktoba 11, 2018 na siku mbili baadaye familia yake ilitangaza donge nono la Sh1bilioni kwa mtu yeyote atakayefanikisha kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.

Akizungumza na MCL Digital,  Gullam Dewji Hussein, baba mzazi wa mfanyabiashara huyo amesema alijulishwa kuwa mwanaye amepatikana akiwa katika gari ambalo lilitelekezwa katika viwanja vya Gymkhana.

Amesema Mo Dewji baada ya kushushwa katika gari hilo alitembea kutafuta msaada wa simu.

Amebainisha kuwa baada ya kupokea simu hiyo alifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kumuona mwanaye.

Kufuatia maelezo hayo ya Gullam  swali linabaki ni nani aliyemsaidia Mo Dewji kupiga simu kwa baba yake, huenda mtu huyo akaramba mamilioni.

Swali hilo pengine litajibiwa vyema na familia ya mfanyabiashara huyo kijana.