Ndege yaanguka ikiwa na abiria 47

Muktasari:

Taarifa za maofisa wa polisi zimesema kuwa ndege hiyo yenye namba PK-661 iliyokuwa ikiruka kutoka mji wa Chitral kuelekea Islamabad ilipoteza mawasiliano kabla ya baadaye kudhibitishwa kuwa ilikua imeanguka.

Islamabad, Pakistan. Ndege ya Shirika la Pakistan imeripotiwa kuanguka kaskazini mwa nchi hiyo ikiwa na abiria 47 muda mfupi baada ya kuanza kuruka. 

Taarifa za maofisa wa polisi zimesema kuwa ndege hiyo yenye namba PK-661 iliyokuwa ikiruka kutoka mji wa Chitral kuelekea Islamabad ilipoteza mawasiliano kabla ya baadaye kudhibitishwa kuwa ilikua imeanguka.

Msemaji wa shirika hilo, Danyal Gilani alisema ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 30 na wengine waliosalia wakiwa wahudumu na marubani.

Katika taarifa yake shirika hilo lilisema ndege hiyo ilikuwa imebeba watu ‘wanaokadiriwa kuwa 40’ lakini taarifa kutoka mamlaka ya anga ilisema kulikuwa na watu 47. Ofisa mwandamizi wa polisi, Laiq Shah alisema ndege hiyo ilianguka katika eneo linalofahamika kama Haveliana.

“ Timu ya waokoaji imeelekea kwenye eneo la tukio nadhani baada ya hapo tutapata taarifa zaidi,” alisikika akieleza msemaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Pervez George wakati akizungumza na Reuters.

Maofisa wa polisi katika eneo hilo waliiambia televisheni ya taifa kuwa ndege hiyo ilianguka katika kijiji kimoja kilichopo kaskazini mashariki mwa Pakistan.

Shirika la habari la AP liliarifu kuhusu kundi la waokoaji kuelekea kwenye eneo la tukio. Moshi mkubwa ulishuhudiwa ukivuka toka eneo ambalo ndege hiyo ilianguka.  Imeelezwa kuwa ndege hiyo ilipoteza mawasiliano dakika 90  tangu ianze kuruka.