Ngorongoro ‘walia’ na uzembe wa Faru Salma

Muktasari:

Lakini usishangae pindi wahifadhi katika hifadhi hiyo watakapokuambia kuwa kuna faru anayeitwa Job Ndugai na mwingine Salma Kikwete. Yupo pia Faru Seleli na Telele.

Arusha. Unapoingia katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, (NCAA) utakutana na wanyama wa aina mbalimbali wanaovutia wakiwamo faru.

Lakini usishangae pindi wahifadhi katika hifadhi hiyo watakapokuambia kuwa kuna faru anayeitwa Job Ndugai na mwingine Salma Kikwete. Yupo pia Faru Seleli na Telele.

Hata hivyo, faru aliyepewa jina la Salma, anatajwa kuwa ni mzembe na asiyejua kutunza watoto wake.

Akizungumza na wanahabari jana, mhifadhi mkuu wa NCAA, Dk Freddy Manongi alisema jina la Faru Salma, lilitolewa kumuenzi Salma Kikwete ambaye ni mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ambaye alipenda zaidi kutembelea hifadhi hiyo mara kwa mara.

Dk Manongi alisema wapo faru wenye majina ya viongozi mbalimbali ambayo walipewa kulingana na mazingira mbalimbali.

Faru wengine waliopewa majina ya viongozi ni Faru Seleli, (mbunge wa zamani wa Nzega, Lucas Seleli); Faru Telele (mbunge mstaafu wa Ngorongoro, Saning’o Ole Telele) na Spika Job Ndugai ambao waliwahi kuwa wajumbe wa bodi ya NCAA.

Akimzungumzia Faru Salma ambaye ni mjamzito kwa sasa, Dk Manongi alisema wanatarajia kumjengea banda maalumu kwa sababu ni mzembe na si mwangalifu katika utunzaji wa watoto ambao huliwa na fisi mara tu anapowazaa. “Ameshazaa mara nne na watoto wake wameliwa na fisi kutokana na uzembe wake, tunamfuatilia kwa karibu ili hii mimba aliyonayo akikaribia kuzaa tunamuweka kwenye banda, mtoto akishakua na kuweza kujihami mbugani, tutamuachia,”alisema Dk Manongi.

Wataka wapewe majina yao

Kadhalika Dk Manongi alizungumzia ongezeko la watu wanaotaka faru wapewe majina yao akisema hamasa hiyo ilianza baada ya majina ya Faru Fausta na John kuwavutia.

Dk Manongi alikuwa akielezea mikakati waliyonayo ya kukuza utalii kupitia vyombo vya habari kama njia ya kuwawezesha wananchi na wageni kufahamu vivutio mbalimbali nchini.

Bila kutaja idadi ya walioomba majina yao wapewe faru, alisema kumekuwa na ongezeko la watu wenye majina makubwa kutamani wanyama hao wanaozaliwa ndani ya Kreta ya Ngorongoro waitwe majina yao jambo wanalolihusisha na elimu ya uhifadhi na utalii kuongezeka.

“Tunapokea maombi mengi, lakini niwaambie kuna gharama kubwa katika kuwahifadhi wanyamapori aina ya faru kutokana na umuhimu wake na mamlaka tunaipitia upya sera ya kutoa majina kwa wanaotaka ili wachangie gharama za uhifadhi,” alisema.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya hifadhi hiyo kinasema kutokana na maombi kuongezeka ambayo hawawezi kuyatosheleza, sera mpya iliyopendekezwa ni faru kupewa jina la mtu aliyechangia shughuli za uhifadhi kwa kiwango kikubwa na awe ameshafariki dunia.

Pendekezo jingine ni kuwa iwapo mtu atahitaji jina lake apewe faru atatoa mchango maalumu utakaowezesha kuendeleza huduma za uhifadhi wa faru.

Hamasa hiyo imekuja baada ya Faru John na Fausta kuwa maarufu zaidi na watu wengi hasa viongozi kuvutiwa majina yao kupewa faru.

Kuhusu Faru Fausta mwenye umri wa miaka 54 anayeaminika ndiye mkongwe zaidi duniani, Dk Manongi alisema kwa sasa afya yake imeimarika lakini ataendelea kuhifadhiwa. Fausta anatajwa kutumia kiasi cha Sh760 milioni kwa mwaka kwa ajili ya kumnunulia chakula ambazo ni nyasi maalumu.