Nyumba 1,300 kuondoka, CCM Kibamba yavunjwa

Tingatinga la Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) likibomoa Ofisi ya CCM Kata ya Kibamba, Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Ubomoaji huo ni wa kupisha hifadhi ya Barabara ya Morogoro inayoanzia Kimara hadi Kiluvya na nyumba zilizo umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya barabara kila upande, zitabomolewa.

Dar es Salaam. Bomoabomoa ni balaa. Imeelezwa kuwa bomoabomoa inayoendelea eneo la Mbezi hadi Kiluvya itazikumba zaidi ya nyumba 1,300 yakiwamo mahekalu ya vigogo, nyumba za ibada na vituo vya mafuta.

Ubomoaji huo ni wa kupisha hifadhi ya Barabara ya Morogoro inayoanzia Kimara hadi Kiluvya na nyumba zilizo umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya barabara kila upande, zitabomolewa.

Mmoja wa wasimamizi wa ubomoaji huo kutoka Tanroads ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema wanatarajia kubomoa nyumba zaidi 1,300, “Tayari tumebomoa nyumba zaidi ya 50 na tunaendelea kubomoa kwani zoezi hili ni endelevu na baadhi ya wananchi wanabomoa wenyewe.”

Msimamizi huyo pia alisema mbali na kubomoa nyumba pia wanawakamata wafanyabiashara wadogo, “Mpaka sasa tumekamata wafanyabiashara zaidi ya 1,000 na tunaendelea kuwakamata. Tunafanya hivi kwa sababu tulishawaambia waondoke katika maeneo haya, lakini wanaonekana kukaidi.”

Alisema wanapowakamata wanawapeleka polisi kwa hatua zaidi za kisheria na wengine hutozwa faini.

Akizungumzia kubomolewa kwa nyumba hizo Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama alisema walitoa notisi kwa nyumba zaidi ya 1,000 zitakazobomolewa katika eneo hilo.

Hali ilivyokuwa

Jana, mwandishi wetu alishuhudia Tanroads wakibomoa baadhi ya nyumba na kuwakamata wafanyabiashara hao na kubomoa baadhi ya majengo hayo yaliyo ndani ya hifadhi ya barabara ikiwamo Ofisi ya CCM Kibamba hali iliyozua taharuki.

Walianzia kwa Hassan Said eneo la Mbezi kwa Msuguri anayefyatua matofali na kubomoa visima viwili vya maji na banda la kuhifadhia vifaa.

Baba wa mmiliki wa eneo hilo, Yusuph Omari alisema hawakupewa taarifa kama wanakwenda kubomoa jana, “Tulishaambiwa tangu zamani tuondoe vitu lakini leo (jana) hawakutwambia kama wanakuja.”

Bomoabomoa hiyo ilihamia Mbezi Mwisho kwa wafanyabiashara ambao walikuwa wamepanga bidhaa zao katika eneo la hifadhi. Waliwakamata pamoja na kutwaa bidhaa zao na kuzipakia kwenye gari la polisi.

“Hawa wanapanga biashara barabarani kiasi ambacho kinaleta usumbufu kwa watembea kwa mguu. Tunawakamata ili kulinda usalama maana wanaweza kusababisha hatari barabarani,” alisema msimamizi wa bomoabomoa hiyo.

Wakati kazi hiyo ikiendelea, wananchi na baadhi ya wafanyabiashara hao walikuwa wakikimbia ovyo. Wapo walioacha vibanda vyao wazi na wengine wakijitahidi kuokoa mali zao kwa kubeba na kukimbia.

Baada ya hapo, safari iliendelea hadi Kibamba CCM. Hapo, kazi ya kubomoa baadhi ya majengo ikiwamo ofisi ya CCM Kata ya Kibamba ilianza.

Akizungumza kabla ya jengo hilo kubomolewa katibu wa chama hicho Kata ya Kibamba, Abdallah Yakub alisema ofisi hiyo haikuwapo ndani ya mita 60, bali sheria ya mita 121.5 ndiyo imewafuata, “Kwa kuwa wametufuata inabidi tulipwe. Awali, walisema watatulipa ila hatujui hadi sasa kama tunalipwa au la.”

Awali, Yakub alisema muda wa kubomolewa kwa jengo hilo waliopewa na Tanroads ulikuwa haujafika hivyo wasingeweza kuligusa jana lakini wakati akisema hayo, lilibomolewa mbele ya macho yake.

Wakati bomoabomoa ikiendelea Kibamba, wananchi walikuwa wakihaha kuhamisha vitu vyao huku wengine wakionyesha kukata tamaa ya maisha.

Mmoja wao, Mwamvita Njau alisema hawajui wanaelekea wapi kwani hawakutarajia kama nyumba yao ingebomolewa jana.

“Tunaishi kama wakimbizi, vitu vyetu vipo nje. Tungelipwa tungeenda kutafuta sehamu nyingine. Tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma. Hatuna kosa, tuliishi hapa miaka mingi basi wangetwambia kwamba sehemu hizi hazitakiwi kujengwa.”

Pingamizi kuamriwa Agosti 30

Wakati bomoabomoa hiyo ikiendelea, hatima ya maombi ya wakazi wa Kimara Stop Over na Mbezi ya kibali cha kufungua kesi ya uwakilishi kupinga kubomolewa kwa nyumba zao kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro sasa itajulikana Agosti 30 Mahakama itakapotoa uamuzi wa pingamizi la Serikali.

Wakazi hao zaidi ya 200 wa Kimara Stop Over na Mbezi, wamefungua maombi Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, wakiomba kibali cha kuwakilishwa na Ephrahim Kavishe na wenzake wanne kufungua kesi kupinga operesheni hiyo.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mmoja wa wajibu maombi hayo amewawekea pingamizi, akiiomba Mahakama iyatupilie mbali maombi hayo huku akianisha kasoro mbalimbali za kisheria.

Jana baada ya mvutano wa hoja za kisheria kwa mawakili wa pande zote, Jaji Crencecia Makuru alipanga kutoa uamuzi wake dhidi ya pingamizi hilo Agosti 30, uamuzi ambao ndiyo utakaotoa hatima ya maombi hayo.

Kama mahakama hiyo itakubaliana na hoja za pingamizi hilo la Serikali, basi huenda ikayatupilia mbali maombi hayo, jambo ambalo litawafanya waanze upya mchakato wa kuomba kibali hicho kabla kufungua kesi ya msingi kupinga bomoabomoa hiyo.

Lakini ikiwa itakubaliana na majibu ya hoja za pingamizi hilo zilizotolewa na wakili waombaji hao na kutupilia mbali hoja za pingamizi la Serikali, mahakama itaanza kusikiliza maombi hayo ya uwakilishi, kisha kutoa uamuzi wa ama kuwakubalia au la.

Imeandikwa na Jackline Masinde, Asna Kaniki, James Magai na Hidaya Nyanga.