Polisi watatu wajiua kwa risasi ndani ya saa 48

Waombolezaji wakilia baada ya kukataliwa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa askari Nelson William

Muktasari:

Konstebo Nelson William (28), alijiua juzi saa tisa alasiri kwa kujipiga risasi 

Dar/Mikoani. Ndani ya saa 48, askari watatu wa Jeshi la Polisi wamejiua kwa kujipiga risasi, mmoja akiacha waraka ukihusisha wivu wa kimapenzi.

Konstebo Nelson William (28), alijiua juzi saa tisa alasiri kwa kujipiga risasi iliyofumua kichwa katika kituo kidogo cha Polisi Natta wilayani Serengeti mkoani Mara kwa sababu ya wivu wa mapenzi na mwili ulisafirishwa jana kwenda Iringa kwa mazishi na askari wengine wawili walijiua mmoja Tabora na mwingine Morogoro.

Taarifa ya polisi inasema Jumanne saa 12 asubuhi askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Tabora, Michael Hosea alijiua kwa kujipiga risasi nne kichwani muda mfupi kabla ya kuelekea lindoni. Jana, pia saa 12 asubuhi, mkufunzi katika chuo cha maofisa wa polisi Kidatu wilayani Kilombero, Benedict Nyamagatara alijiua kwa risasi.

Tukio la Morogoro

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbrod Mutafungwa alisema Nyamagatara aliyekuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi alijipiga risasi kwenye taya na kutokea kichwani.

Alisema ofisa huyo alikuwa zamu akiwakagua askari wengine na kutoa maelekezo ya kazi ndani ya chuo. Alisema alitumia silaha ya mmoja wa askari kujipiga risasi.

Kamanda Mutafungwa alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Kiwanda cha Sukari Kilombero One (K1) na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Tabora

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Graifton Mushi alisema askari wa FFU Hosea alijiua kwa kujipiga risasi nne baada ya kuiweka bunduki aina ya SMG shingoni.

Alisema awali, askari huyo alichukua bunduki katika ghala kuelekea lindoni Benki ya Access mjini Tabora umbali wa kilomita moja na nusu kutoka kituo cha FFU.

Kamanda huyo alisema chanzo cha kujiua askari huyo hakijajulikana na uchunguzi unaendelea akibainisha mara nyingi matukio ya aina hiyo hutokana na msongo wa mawazo.

Alisema ni vizuri watu wanapokuwa na tatizo waeleze ili kupatiwa ushauri au kusaidiwa kuliko kukaa kimya na hatimaye kuchukua uamuzi wa kujiua.

Askari aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini alisema Hosea alionekuwa kuwa mtu mwenye mawazo mengi katika siku za hivi karibuni.

Waraka haujasomwa

Katika tukio la Serengeti, inadaiwa kuwa konstebo William (28) aliacha waraka akitaka usomwe wakati mwili wake ukiagwa akieleza kuwa sababu ya kujiua ni mgogoro kati yake na mpenzi wake. Hata hivyo, ujumbe huo haukusomwa jana.

Mwanamke aliyetajwa katika waraka huo (jina linahifadhiwa) hakufika kuaga mwili ikielezwa na ndugu zake kuwa hali yake kiafya si nzuri. Mwili wa askari huyo uliagwa katika hospitali teule ya Wilaya ya Mugumu.

Baadhi ya askari wakizungumza kwa sharti la majina yao kutotajwa walidai kuwa mwenzao hakufurahishwa na uamuzi wa viongozi wao kumlazimisha kulipa vyombo alivyovunja wakati wa ugomvi na mpenzi wake kwa kuwa vilikuwa mali yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki alisema hakuna anayeshikiliwa kuhusiana na tukio la kujiua kwa askari huyo na kwamba wanaendelea kufuatilia waraka unaodaiwa kuwa aliuandika.

Imeandikwa na Anthony Mayunga (Serengeti), Robert Kakwesi (Tabora) na Lilian Lucas (Morogoro).