Polisi watupiana mpira upekuzi ofisi za Chadema

Baadhi ya Viongozi wa Chadema wakitoka katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam jana kuitikia wito wa jeshi hilo.
Walioitikia wito huo ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (kushoto), Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (wa pili kushoto), Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (aliyevaa kofia) na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (kulia). Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Wakati Chadema wakidai kuwa askari wa jeshi hilo walikwenda ofisini hapo juzi saa moja usiku kwa lengo la kufanya upekuzi, si Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Boaz; Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa; wala Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliyekuwa tayari kulizungumzia.

Viongozi wa Jeshi la Polisi wametupitia mpira juu ya taarifa za askari wake kwenda ofisi za makao makuu ya Chadema Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanya upekuzi.

Wakati Chadema wakidai kuwa askari wa jeshi hilo walikwenda ofisini hapo juzi saa moja usiku kwa lengo la kufanya upekuzi, si Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Boaz; Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa; wala Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliyekuwa tayari kulizungumzia.

Juzi usiku, Chadema ilitoa taarifa kuhusu tukio hilo ikisema polisi walifika katika ofisi zao wakiwa na magari matano wakijitambulisha kuwa ni kutoka ofisi za upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ya mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje, John Mrema ilisema polisi waliwajulisha walinzi kuwa wanataka kufanya upekuzi kwenye ofisi lakini hawakuwa na hati ya upekuzi na hawakufuatana na viongozi wa serikali ya mtaa kama sheria inavyotaka.

“Walinzi wetu waliwakatalia kwa kuwa hawakufuata utaratibu na wala hawakueleza wanataka kupekua nini ndani ya ofisi zetu. Tunalaani kitendo hiki na tunajiuliza ni kwa nini wamekuja usiku na ikiwa ni siku moja tu baada ya polisi kufanya uvamizi kama huo kwa CUF Zanzibar na kufanya upekuzi,” alihoji Mrema.

Alipotafutwa ili kuzungumzia ukweli wa taarifa hiyo ya Chadema, Kamanda Mambosasa alisema, “Sijaletewa taarifa za waliokwenda kwani waliokwenda ni makao makuu wale.”

Msemaji wa jeshi hilo, Mwakalukwa alisema asingeweza kulizungumzia kwa kuwa alikuwa safarini akitokea Kigoma kuelekea Dar es Salaam.

“Ofisi ni taasisi, kuna IGP, DCI na kuna msemaji wa Jeshi la Polisi ambaye ni mimi ila nipo safarini natoka Kigoma na kesho (leo) nitakuwa ofisini. Watafute IGP au DCI,” alisema Mwakalukwa.

DCI Boaz alipopigiwa simu na kuelezwa kuhusu suala hilo alisema apewe muda aulize kwa kuwa halifahamu.

Baada ya muda alipiga simu mwenyewe na kusema, “Masuala ya mikoani yanashughulikiwa na makamanda wa mikoa yao. Jitahidi umpate Mambosasa atakupa taarifa kwa maandishi. Makao makuu tunashughulika na sera na mambo makubwa si madogo madogo kama hayo.”

Waachiwa kwa dhamana

Jana mchana, viongozi wanne kati ya saba wa chama hicho waliripoti Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuitikia wito wa jeshi hilo, huku wakitoa sababu ya mwenyekiti, Freeman Mbowe; katibu mkuu, Dk Vincent Mashinji; na naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu kushindwa kuripoti.

Walioripoti jana kituoni hapo saa 6:10 mchana na kuachiwa kwa dhamana saa 7:45 mchana kwa dhamana ni, naibu katibu mkuu-Bara, John Mnyika; mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee; mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche; na Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.

Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Kibamba akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema kupitia wakili wao, Peter Kibatala walipewa dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni hapo Februari 27.

Wito wa Polisi kwa viongozi hao, ulitolewa juzi ikiwa ni siku nne kupita tangu kutokea kwa kifo cha Akwilina Akwiline, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Kifo cha Akwilina kinadaiwa kuwa kimetokana na kupigwa risasi na polisi Februari 16 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.

Sababu za Mbowe, Dk Mashinji

Mbowe, Dk Mashinji na Mwalimu hawakufika kuripoti polisi ikielezwa na Mrema ni kutokana na kuwa nje ya Dar es Salaam.

“Mfano, Salum Mwalimu jana alitangulia Mafinga (Iringa) kwa ajili ya kuongoza mazishi ya kiongozi wetu Daniel John hivyo kwa wito tuliopokea asingeweza kufika sawa na mwenyekiti (Mbowe) alikuwa nje ya Dar es Salaam,” alisema Mrema.

Alisema Dk Mashinji wakati wito wa kuripoti polisi ukitolewa alikuwa safarini kwenda Marekani.

Somo la Sumaye kwa viongozi

Mbali na matukio hayo, katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Anna lililoko Hananasif jijini Dar es Salaam, kulifanyika ibada ya kumwombea Daniel John (37) aliyekuwa katibu wa Chadema, Kata ya Hananasif, ambaye mwili wake uliokotwa Coco Beach baada ya kutokweka Februari 11.

John aliyezaliwa Desemba 26, 1980 ameacha watoto wawili na mjane mmoja, Paulina Vitalis na jana mwili wake ulisafirishwa kwenda Mafinga mkoani Iringa kwa mazishi yatakayofanyika leo.

Katika ibada iliyohudhuriwa na viongozi wa Chadema, wanachama na waombolezaji wengine, mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chadema na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alitoa wito kwa viongozi wa Serikali na dini kuhakikisha wanajenga umoja na kukemea uvunjifu wa amani.

“Haki haitendeki, maumivu yanatokea na tunanyamaza, tunapaswa kutupwa nje na kukanyagwa, Daniel amekuwa chumvi hivyo ametupwa nje. Mungu alitoa na Mungu ametwaa lakini sisi binadamu tunafanya mambo yasiyostahili kama hili lililotokea kwa Daniel,” alisema.

Sumaye alisema, “Katika kupigania haki, kuna wachache watamwaga damu, Daniel ni miongoni mwao na hao hawatarudi, hakuna historia hiyo popote ila damu hiyo itadai siku zote.”

Kuhusu viongozi wa kiroho alisema, “Viongozi wa dini kemeeni, mnapoona kuna ubaya halafu hamsemi, mnabaki kusema hii si siasa, kemeeni ni jukumu letu sote na msipokemea taifa hili linakwenda kubaya.”