Profesa Kabudi azungumzia utekelezaji wa ahadi za Rais Magufuli

Waziri wa Katiba  na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi 

Muktasari:

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amezungumzia mafaniko mbalimbali ya Serikali, akieleza kuwa Rais John Magufuli katika uongozi wake tangu mwaka 2015 ameweza kufanya mambo mengi mazuri


Dar es Salaam. Waziri wa Katiba  na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amemwagia sifa Rais John Magufuli akieleza kuwa ametekeleza ahadi zake vyema tangu alipoapishwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi Novemba 5, 2015.

Profesa Kabudi ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba Mosi, 2018 wakati akizungumza katika kongamano la siasa la uchumi lililofanyika Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM).

Akieleza mafanikio hayo amesema lengo la Serikali ni pamoja na kuendelea kukuza uchumi na kupunguza umasikini, kujenga mazingira wezeshi na uwekezaji, kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii, kujenga nidhamu ya utendaji kazi na kuimarisha uhusiano wa kimataifa.

“Uchimbaji wa madini umeongezeka mpaka asilimia 14.5, mawasiliano asilimia 13.8. Mapato ya ndani ya kodi yameongezeka kutoka Sh12,334 bilioni hadi Sh15,191 bilioni mwaka 2017/18 huku makusanyo ya kodi kwa jumla yakifikia wastani Sh1.2 trilioni kwa mwezi mwaka 2018 ikilinganishwa na Sh800 bilioni mwaka 2015,” amesema.

Kuhusu mradi wa umeme wa Stiegler’s gorge, Profesa Kabudi alisisitiza kuwa utafanyika licha ya kukosolewa na wadau wa mazingira na utalii.

“Niseme bila tashwishi utatekelezwa ije mvua lije jua, utatekelezwa. Wapende wasipende utatekelezwa, watake wasitake utatekelezwa. Kelele zitakuwa nyingi lakini utatekelezwa,” amesema.

Amesema wakati wa Mwalimu Julius Nyerere mradi huo ulishindikana kutokana na kukosekana fedha.

Amesema  mafanikio mengine ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kusisitiza kuwa iliyopo sasa haitang’olewa.

Kuhusu ununuzi wa ndege, amesema licha ya kubezwa na baadhi ya watu lakini zimenunuliwa ndege mbili aina ya Airbus A 220300 zinatarajia kuingia nchini Novemba, 2018 ndege ya pili ya Dreamliner ikitarajiwa kuwasili nchini mapema 2020.

Pia, aligusia bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima hadi Tanga, “Mnaotoka Tanga hata bomba halijaisha lakini hali ya vuguvugu la uchumi wa Tanga imebadilika.

Ujenzi na madaraja makubwa, mhuri wake ni Magufuli. Tumeona Mfugale Flyover (daraja la juu la Tazara jijini Dar es Salaam) na sasa tunaona ujenzi wa interchange ya Ubungo (barabara ya juu ya Ubungo).”