Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mradi wa Sh529.5 milioni wa Shule ya Msingi Nduli wakamilika, kunufaisha wanafunzi 820

Muktasari:

  • Wanafunzi zaidi ya 820 wa Manispaa ya Iringa wanatarajiwa kunufaika na mradi wa Sh529.5 milioni wa Shule ya Msingi Nduli uliotekelezwa kupitia BOOST. Mradi huo umejumuisha madarasa, nyumba ya walimu, vyoo na jengo la utawala, ukilenga kuboresha mazingira ya elimu na kupunguza msongamano wa wanafunzi.

Iringa. Zaidi ya wanafunzi 820 wa Manispaa ya Iringa wanatarajiwa kunufaika na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia baada ya Serikali kukamilisha mradi wa ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Msingi Nduli wenye thamani ya Sh529.5 milioni.

Mradi huo, uliotekelezwa kupitia Mpango wa BOOST, umehusisha ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa ya shule ya msingi, madarasa mawili ya elimu ya awali, jengo la utawala, nyumba ya walimu ya familia mbili pamoja na matundu 18 ya vyoo.

Katibu wa NEC wa CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi amepongeza utekelezaji wa mradi huo akisema unaonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

Akizungumza leo Juni 20, 2026 wakati wa ukaguzi wa mradi huo katika Kata ya Nduli, Manispaa ya Iringa, Kihongosi amesema Serikali chini ya Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia.

“Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha sekta ya elimu kwa kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia. Hapa Nduli matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana wazi,” amesema Kihongosi.

Amesema ameridhishwa na ubora wa kazi iliyofanyika, akibainisha kuwa miundombinu yote imejengwa kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilika kwa wakati.

“Naufahamu vizuri mradi huu kwa kuwa ni mkazi wa Nduli. Nimeridhishwa na ubora wa kazi iliyofanyika kwani miundombinu yote imejengwa kwa viwango vinavyostahili. Mradi huu utakuwa mkombozi kwa wanafunzi wengi wa eneo hili,” amesema.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, akizungumza na wananchi na baadhi ya viongozi wakati wa ukaguzi wa mradi wa Shule ya Msingi Nduli, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa. Picha na CCM.

Kihongosi amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule za jirani na kuongeza fursa za watoto kupata elimu katika mazingira bora na salama.

Aidha, amewataka wananchi kushiriki katika kulinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Pia, amewahimiza wazazi na walezi kuendelea kuwalea watoto katika maadili mema na kuwahamasisha kusoma kwa bidii.

Awali, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Isaya Lalika, amesema mradi ulianza kutekelezwa Septemba 5, 2025 na kukamilika Juni 9, 2026 baada ya Serikali kutoa fedha kupitia Mradi wa BOOST.

Lalika amesema pamoja na mafanikio hayo, shule bado inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji, hivyo ameomba Serikali kusaidia ujenzi wa kisima ili kuhakikisha wanafunzi na walimu wanapata huduma ya maji safi na salama.

“Upatikanaji wa maji utasaidia pia shughuli za kilimo cha mazao ya lishe na matunda kwa ajili ya wanafunzi,” amesema.

Mbali na kukagua mradi huo, Kihongosi alipanda miti katika eneo la shule kama sehemu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pia, alitembelea Shina namba 10 Mafifi katika Kata ya Kihesa na kuzindua Kituo cha Usafirishaji wa Bodaboda cha Mlandege kilichopo Kata ya Kwakilosa, Manispaa ya Iringa.

Baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na kukamilika kwa mradi huo, wakisema utachangia kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wao.

Mkazi wa Nduli, Rehema Mwakalinga, amesema madarasa mapya yataondoa tatizo la msongamano wa wanafunzi lililokuwepo kwa muda mrefu.

Naye dereva wa bodaboda wa Kituo cha Mlandege, Juma Mgaya, amesema uwekezaji wa Serikali katika elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, mkazi wa Kihesa, Mzee Peter Mhando, ameomba Serikali kuendelea kupeleka miradi mingine ya maendeleo ikiwemo maji na barabara ili kuendana na maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta ya elimu.