RC Iringa aanza utekelezaji agizo la Rais Magufuli

MASENZA ASHUSHA AGIZO LA MAGUFULI KWA WALIO CHINI YAKE

Muktasari:

Masenza amewataka walimu wakuu wa shule zote mkoani kwake kuandika barua kueleza aina ya michango iliyopo shuleni kwao na sababu za uwepo wake.

Iringa. Siku moja baada ya Rais John Magufuli kupigilia msumari wa mwisho suala la michango kwa wanafunzi mashuleni, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amewataka walimu wakuu wa shule zote mkoani kwake kuandika barua kueleza aina ya michango iliyopo shuleni kwao na sababu za uwepo wake.

Masenza ameonya mwalimu ambaye atatoa taarifa za uongo katika barua yake hatua zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo ya kuondolewa katika nafasi yake.

"Kwenye waraka ambao kila mtu anao unazungumzia elimu bila malipo, tayari Serikali ilishaelekeza namna ya kuendesha elimu bila malipo, waraka namba 3 wa 2016 unaozungumzia elimu bila malipo na waraka wa elimu namba 8 wa 2011 kuhusu michango mbalimbali wanayopaswa kutoa wazazi kupitia kamati na bodi za shule," amesema Masenza na kuongeza;

"Mimi ninajua katika kamati na  bodi za shule ninyi ni makatibu, ikifika katika jambo hili, tafadhali kila mwalimu aone hahusiki na jambo lolote linalozungumzia michango katika shule za msingi na sekondari na kama kuna hitaji lolote libainishwe na jamii," amesema.

Amesema shule ni za jamii na jamii ikibainisha yenyewe nje ya utaratibu wa mwalimu mkuu juu ya nini wanataka kufanya na kusimamia wao wenyewe hilo linaruhusiwa.

"Sasa nimewaita ili nijiridhishe, nitamtaka kila mwalimu mkuu wa shule kwa mkono wake mwenyewe aandika barua ya kueleza kama shule yake ina mchango ama la na barua sote ziandikwe kwa mkuu wa mkoa," amesema Masenza.

Masenza amesema barua hizo zitapitiwa na ofisi yake na kisha ukaguzi utafanyika katika kila shule  zikihojiwa kamati na bodi za shule kubaini michango kama ipo sababu za uwepo na namna amehusika kuwepo kwa michango hiyo.

Katika hatua nyingine mkuu huyo amewaagiza wakuu wa shule kuwapokea wanafunzi wote wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza bila kujali wana sare za shule ama la.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa amewataka wakuu wa shule zote za binafsi mkoani humo kuwarejesha wanafunzi waliowaondoa shuleni mwao kutokana na kutofikia wastani wa ufaulu wanaoutaka la sivyo shule zao zitafungwa.