RC atangaza kiama wanaoipaka Serikali tope

Muktasari:

Makalla ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wafanyabiashara na wamiliki wa wa hoteli walipokutana   kwenye uzinduzi wa hoteli ya kisasa ya Mgwasi Inn iliyopo Mama John Jijini Mbeya.

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amewatangazia kiama watu watakaobainika   kuipaka tope na kutaka kuichonganisha Serikali na wafanyabiashara kwa kuwakadiria na kuwatoza kiwango cha kodi ambayo ni kinyume na matakwa halisi.

Makalla ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wafanyabiashara na wamiliki wa wa hoteli walipokutana   kwenye uzinduzi wa hoteli ya kisasa ya Mgwasi Inn iliyopo Mama John Jijini Mbeya.

Amesema kuna watu hususani watumishi wasiokuwa wamaaminifu wamekuwa wakiipaka tope Serikali kwa wafanyabiashara na   kuleta chuki na kuiona sio rafiki kwa mfanyabiashara  kutokana na kuwakadiria kodi isiyoendana na uhalisia wa biashara yenyewe  huku akisisitiza kodi ilipwe kwa kiwango halali na si vinginevyo.

“Jamani  isionekana mtu kufanya biashara ni adhabu   kwa  kutwishwa zigo kubwa la kodi. Na wengine wanaipaka tope Serikali ‘eti Serikali hii ni ya hapa kazi tu’ hivyo tumekukadiria kodi hiyo ni lazima ulipe...Hapana hatuendi  hivyo na ninaamini tumeshaelekezana watu watalipa kodi kwa mujibu wa sheria na kwa viwango stahiki na si vinginevyo,” amesema Makalla.