ACT Wazalendo yapaza sauti bajeti ndogo Wizara ya Maji

Waziri Kivuli wa Maji wa chama cha ACT Wazalendo,Yasinta Awati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu bajeti ya Wizara ya Maji iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Maji, Juma Aweso. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema suala la ufinyu wa bajeti ya Wizara ya Maji litajadiliwa kati ya Kamati ya Bajeti na Serikali.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimedai bajeti ya Wizara ya Maji ya 2024/24 iliyowasilishwa bungeni, haiakisi mpango wa wizara hiyo katika utekelezaji wa kufikisha huduma kwa Watanzania.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema suala la ufinyu wa bajeti ya Wizara ya Maji litajadiliwa kati ya Kamati ya Bajeti na Serikali.

Jana Alhamisi Mei 10, 2024 Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliwasilisha bajeti ya wizara hiyo akiliomba Bunge kuidhinisha Sh627.7 bilioni kwa mwaka 2024/25 ambazo tayari zimepitishwa.

Hata hivyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ilisema bajeti hiyo imepungua, hali inayoonyesha Wizara ya Maji si miongoni mwa vipaumbele vya Serikali kwa mwaka huo wa fedha.

Kamati ilisema licha ya kuunga mkono bajeti hiyo, lakini kupungua kwa bajeti ya maendeleo ya wizara kunaweza kuathiri utekelezaji bora wa miradi kwa kukosa tija iliyokusudiwa kwa wananchi.

“Ni mtazamo wa kamati kwamba, kupungua kwa kiasi hiki cha bajeti ya maendeleo kutaathiri utekelezaji wa miradi iliyopangwa kutekeleza kwa mwaka wa fedha 2024/25,” alisema Jackson Kiswaga, ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo alipowasilisha taarifa ya kamati hiyo.

Waziri wa Kivuli wa Maji wa ACT Wazalendo, Yasinta Awati akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 10, 2024 amesema bajeti hiyo ni pungufu kwa Sh128.5 bilioni sawa na asilimia 17 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana 2023/24.

“Kwa mwenendo wa bajeti kushuka kunaonyesha kero kuhusu huduma za maji mijini na vijijini zitaendelea kuwepo kwa miongo kadhaa mbele,” amesema.

“Uchambuzi wetu ACT Wazalendo unaonyesha mwenendo huu wa bajeti haulengi kumaliza tatizo la maji nchini, kwani miradi mingi haijakamilika, hata ile iliyokamilika baadhi haitoi maji,” amesema.

Kutokana na hilo, Awati amesema ACT Wazalendo inaitaka Serikali kuongeza bajeti ya kutosha katika wizara hiyo ili kuondoa kero ya maji nchini.

Ameshauri kutengwa Sh10 trilioni kwa miaka mitano kukamilisha mchakato huo.

Awati amesema chama hicho, kinaunga mkono hatua ya mfumo wa malipo kabla ikiitaka Serikali kugharamia mita hizo na kuwafungia wananchi wanaolipia huduma za maji.

“Serikali itengeneze bei elekezi na nafuu ya kuunganishwa na huduma ya maji mijini na vijiji, ili kurahisisha wananchi kupata maji katika makazi yao,” amesema Awati.