Risiti za EFD zamuingiza matatani mganga mfawidhi

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari juzi Alhamisi ofisini kwake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji huo, Abel Shija alisema katika zahanati hiyo kulikuwa na ukarabati wa jengo la wagonjwa wasiolazwa (OPD) huku zaidi ya Sh4 milioni zikitumika kununulia vifaa bila wahusika kupatiwa stakabadhi za EFD.

Kahama. Matumizi ya mashine za kodi za kielektroniki (EFD) katika Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, yamemtia matatani Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kagongwa, Amina Sophian baada ya kutuhumiwa kutumia fedha za ukarabati bila kutoa stakabadhi za mashine hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi Alhamisi ofisini kwake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji huo, Abel Shija alisema katika zahanati hiyo kulikuwa na ukarabati wa jengo la wagonjwa wasiolazwa (OPD) huku zaidi ya Sh4 milioni zikitumika kununulia vifaa bila wahusika kupatiwa stakabadhi za EFD.

Pia, alisema Sh2.9 milioni zimetumika kumlipa fundi kiwango ambacho hakilingani na kazi iliyofanyika.

“Mchakato mzima unaonyesha kugubikwa na udanganyifu. Halmashauri ilitoa Sh11 milioni za ukarabati wa jengo hilo,” alisema mwenyekiti huyo. Aliwataja wahusika wengine kwenye tuhuma hizo kuwa ni fundi ujenzi, Mayunga Mabala, Francis Kipiga na Elizabeth Raphael waliokuwa wajumbe wa kamati ya ujenzi wa jengo hilo linalodaiwa kukarabatiwa chini ya kiwango huku zaidi ya Sh7 milioni kati Sh11 milioni zikiwa zimetumika. Mhandisi wa idara ya ujenzi katika halmashauri hiyo, Falis Maghembe alisema baada ya kufanya uchunguzi kitaalamu, wamebaini ukarabati huo umefanyika chini ya kiwango ikilinganishwa na fedha zilizotumika.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati hiyo ya Kagongwa, Sophian alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, alimtupia lawama mhasibu aliyekuwa akifanya manunuzi pamoja na malipo na kudai hahusiki katika matumizi ya fedha hizo.

Fundi Mabala, aliyekuwa akisimamia ukarabati huo alidai kuwa kazi zote alizifanya kwa kupatiwa maelekezo na kamati ya ujenzi pamoja na mganga mkuu. Alidai kuwa hata mawe yaliyotumika yalikuwa ni tripu tatu pekee na yalijengewa shimo la kutupia taka. “Ukarabati wa sakafu ulihitaji mawe lakini hayakuletwa, nikaambiwa nitumie mchanga,” alidai fundi huyo.