Roma Mkatoliki, wenzake watekwa

Msanii wa muziki wa kizazi kipya Roma Mkatoliki

Muktasari:

Kaka wa msanii huyo, Omary Mussa alisema watu hao walikuwa wamevaa kiraia na wawenda kwenye studio za Tongwe Records saa 1:30 usiku wakiwa kwenye gari jeusi aina ya Toyota Noah.

Dar es Salaam.  Imedaiwa kuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Mussa maarufu kama ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake watano wamekamatwa na watu eneo la Masaki jijini hapa na kupelekwa kusikojulikana.

Kaka wa msanii huyo, Omary Mussa alisema watu hao walikuwa wamevaa kiraia na wawenda kwenye studio za Tongwe Records saa 1:30 usiku wakiwa kwenye gari jeusi aina ya Toyota Noah.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Susan Kaganda alisema, “Sina taarifa zozote za tukio hilo, ngoja nifuatilie, then nitatoa taarifa.”

Habari za kukamatwa kwa msanii huyo zilitolewa na mwenzake ambaye pia ni mbunge wa Mikumi, Joseph Haule (Profesa Jay) aliyeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: “Nimeshtushwa kusikia kwamba kuna watu wamevamia studio ya Tongwe Records majira ya saa moja usiku na wamemchukua Roma, Mony na kijana wa kazi na pia, wamechukua computer ya studio na screen (Tv) na wameondoka navyo kusikojulikana. Mpaka sasa hatujui wamewapeleka wapi!”