Saa 34 bado Mo Dewji hajapatikana

Muktasari:

Ilipofika saa 9:30 alasiri leo Alhamisi, mfanyabiashara maarufu wa Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo’ alikuwa ametimiza saa 34 tangu atekwe na Wazungu wawili katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.


Dar es Salaam. Mpaka saa 9:55 alasiri ya leo Ijumaa, Mohammed Dewji ametimiza saa 34 tangu alipotekwa Alhamisi asubuhi katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

Polisi wanafanya jitihada kumtafuta bilionea huyo wa Tanzania, ambaye  tangu alipotekwa amezua maswali miongoni mwa jamii wakitaka kujua sababu ambazo zimesababisha kutekwa.

Hali ya taharuki imeendelea kutanda miongoni mwa kada zote nchini, huku suala la usalama wa watu wa kawaida likiwa mjadala na hasa kutokana na kutekwa kwa bilionea huyo ambaye amewekeza katika klabu ya Simba Sh20 bilioni.

Dewji ambaye miaka mitatu iliyopita jarida la Forbes lilimtaja kuwa tajiri namba moja Afrika kwa vijana walio chini ya miaka 40 alitekwa na Wazungu wawili waliomvizia alipokuwa akishuka kwenye gari lake ili aingie kwenye mazoezi kwenye gym ya Hoteli ya Colosseum.

Taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa Sh3.5 trilioni zilianza kusambaa Alhamisi saa 1:00 asubuhi katika mitandao ya kijamii, kabla ya polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kuthibitisha saa mbili asubuhi.

Mwananchi ambayo siku yote ya Alhamisi ilikuwa imepiga kambi katika hoteli hiyo iliwaona  watu mbalimbali wakiwa wamejaa katika geti la kuingia hotelini hapo wakiwemo waandishi wa vyombo mbalimbali waliokuwa wamezuiliwa nje ya geti.

Hotelini hapo kulikuwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa pamoja na maofisa kadhaa wa usalama.

Ulinzi ulikuwa mkali kwa dakika kadhaa, wakati maofisa wa polisi wakifanya uchunguzi wa awali kwa kutumia vipimo, baadhi wakiwa na glovusi mikononi.

Simulizi ya kutekwa

Hali ya simanzi, dua na sala vilitawala katika vinywa vya wanafamilia, wanasiasa, wanamichezo, wanaharakati na wananchi wa kawaida waliolaani vikali tukio hilo.

Mo alitekwa akiwa na gari lake la Range Rover nyeusi, lakini maswali mengi ni kuwa maeneo ya Oysterbay ambako tukio hilo limetokea wanaishi watu wa kipato kikubwa na viongozi wakubwa serikalini, huku ulinzi ukiwa wa uhakika.

Hoteli ya Colosseum inayolindwa na kampuni ya ulinzi ya G1, inapatikana umbali wa takribani kilometa mbili kabla ya kuingia barabara kuu ya Ali Hassan Mwinyi.

Mambosasa aliwaambia waandishi wa habari kuwa ndani ya uzio wa hoteli hiyo kulikuwa na gari huku jingine likiwa nje na wakati Mo alipofika na gari lake, gari la ndani liliwasha taa kuwapa ishara wenzao wa nje walioingia na kumteka Mo.

Anasimulia kuwa MO alipoteremka katika gari,Wazungu wawili waliteremka katika gari lao na kumchukua kwa nguvu kisha kumweka ndani ya gari lao aina ya Toyota Surf kabla ya kuondoka.

Waliondoka kupitia geti la upande wa kushoto, kabla ya kukuta geti limefungwa na kwa sababu mlinzi aligoma kufungua geti walipiga risasi juu kabla ya mmoja wao kushuka kwenye gari na kwenda kufungua mlango yeye mwenyewe.

Msako kila kona

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilitangaza rasmi msako kwa watekaji hao usiku na mchana kupitia hoteli zote kubwa za jiji hilo na leo Ijumaa magari ya polisi yameonekana yakipiga yakirandaranda maeneo ya Masaki na Oysterbay.

Makonda ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa huo, amewahi kuwa mmoja kati ya watumiaji wa gym ya hotel hiyo.

Kwa upande wa familia yake, ndugu hawakuwa tayari kuzungumzia jambo lolote kuhusu tukio la kutekwa kwa MO , Mwananchi ilifika nyumbani kwa mfanybiashara huyo eneo la Masaki na kukuta ulinzi mkali.

Walinzi waliokuwa siku ya tukio hapo nyumbani kwa MO Dewji walichukuliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi kama ilivyo wenzao wa Collessium Hotel na baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo.

Alhamisi pia, msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara alitoa taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo kuhusu tukio la kutekwa kwa mwekezaji huyo.

Manara alisema uongozi wa Simba unawaomba mashabiki kuwa na utulivu, kuomba dua na sala ili mfanyabiashara huyo apatikane.

Huduma zinaendelea hotelini

Huduma za hoteli zinaendelea kutolewa kama kawaida, lakini wamiliki hawakuwa tayari kuzungumza na Mwananchi. Huduma za gym hotelini hapo, zilisitishwa kutwa nzima ya Alhamisi kabla ya kurejeshwa leo Ijumaa.

Ni zaidi ya saa 34, tangu ilipofika saa tisa alasiri na bado mfanyabiashara huyo alikuwa bado hajapatikana, ila polisi wanaendelea na uchunguzi.

Soma zaidi: