Samia awataka wananchi kutunza mradi wa maji

Muktasari:

Mradi huo utakapokamilika utawanufaisha wakati zaidi ya 21,000.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa maji wa Kiloleni wilayani Busega unaogharimu zaidi ya Sh1.6 bilioni na kuwataka wananchi kuitunza miundombinu yake kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Utakapokamilika, mradi huo utanufaisha wakazi zaidi ya 21, 000 wa kata ya Kiloleli.

Akizungumzia maendeleo ya sekta ya pamba, Makamu wa Rais amewahakikishia wakulima wa zao hilo uhakika wa viuadudu akisema tayari Serikali imetoa fedha za kuagiza chupa za kutosha ambazo zimeanza kusambazwa kwa wakulima vijijini tangu mwanzoni mwa mwezi huu.

“Awamu ya pili ya dawa inatarajiwa kuwasili wiki ijayo, wakulima hawapaswi kuwa na hofu ya dawa ya kuulia wadudu wanaoshambulia pamba,” amesema Makamu wa Rais.

Akiwa kwenye ziara ya kukagua mashamba ya pamba wilayani Igunga Februari 4, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh10 bilioni kwa ajili ya kununua na kusambaza viuadudu.

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini (TCB), Marco Mtunga, hadi kufikia Aprili, zaidi ya chupa milioni sita za viuadudu zitakuwa zimesambazwa kwa wakulima.

Mtunga anasema chupa milioni tisa za viuadudu zenye gharama ya Sh36 bilioni zinatarajiwa kutumika katika msimu huu.

Wakati Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka ameahidi kuwa Serikali inakusudia kufunga taa za barabarani katika mji wa Ramadi, mbunge wa Busega, Rafael Chegeni yeye ameiomba Serikali kuupa Ramadi hadhi ya kuwa mji mdogo kutokana na kuwa na mapato yanayomudu kugharamia shughuli na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.