Serikali kujenga’ flyover’ nyingine saba Dar

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Barabara hizo zinatarajiwa kujengwa katika maeneo ya Chang’ombe, Uhasibu, Mwenge, Morocco, Kamata, Magomeni na Tabata.

Dar es Salaam. Serikali imesema mwaka huu itakamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa barabara saba za juu (flyover) katika jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza foleni.

Barabara hizo zinatarajiwa kujengwa katika maeneo ya Chang’ombe, Uhasibu, Mwenge, Morocco, Kamata, Magomeni na Tabata.

“Matumaini yetu ni kuwa ifikapo Juni mwaka huu upembuzi huu utakuwa umekamilika,” Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema alipokuwa akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.

Dk Abbasi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo), alisema jana katika mkakati huo wa kupunguza foleni, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya usafiri ikiwamo kuanza awamu nyingine ya ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka utakaoanzia Barabara ya Kilwa hadi Mbagala na mwingine ukianzia Uhuru hadi Gongo la Mboto.

Mpango wa ujenzi wa flyover hizo unakuja huku tayari Serikali ikiwa imeshaanza kujenga nyingine mbili; ya Tazara ambayo inakaribia kukamilika na ya Ubungo ambayo ipo katika hatua za awali za kujengwa.

Alisema wakati kazi ya ujenzi wa barabara hiyo eneo la Ubungo ikiendelea vizuri, ile ya Tazara inatarajiwa kuanza kutumika ifikapo Oktoba.

Dk Abbasi alisema Serikali imeendelea kung’ara katika ripoti za kimataifa kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya wananchi.

Alisema ripoti zilizotolewa hivi karibuni, zinaitaja Tanzania kuwa siyo tu inafanya vizuri katika maendeleo ya kiuchumi, bali pia iko kwenye mwelekeo unaoeleweka katika kipengele kinachohusu utawala bora.

Alisema ripoti ya Jarida la Economics iliyotolewa Februari 5, iliiorodhesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika kipengele cha utawala bora ikishika nafasi ya kwanza katika eneo la Afrika Mashariki wakati duniani ikiwa ya 91 na Kenya ya 95.

Alisema ripoti nyingine ya Foresight Afrika iliyotolewa hivi karibuni, inasema Tanzania ni moja kati ya nchi chache barani Afrika ambayo itakuwa na uchumi imara katika kipindi cha mwaka 2018.

Dk Abbasi alisema Serikali inazingatia utekelezaji wa uchumi jumuishi na ndiyo maana imekubalika katika taasisi za kimataifa, “Hizi ripoti zinaendelea kuthibitisha namna Serikali inavyoendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake maana hata ukiangalia ripoti ya Foresight Afrika, inaonyesha tunashika nafasi ya tano kwa kuwa na uchumi mzuri tukitanguliwa na Ghana, Ethiopia, Ivory Coast na Senegal.”

Pia Dk Abbasi alisema tangu mwaka 2015 hadi sasa, Serikali imeongeza bajeti ya afya kutoka Sh86 bilioni hadi Sh269 bilioni na kuwezesha upatikanaji wa huduma mbalimbali na vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya ambazo awali zilikuwa hazipatikani nchini.

“Tuna mpango pia wa kusambaza umeme katika vijiji karibu 3,599 achilia mbali miradi mikubwa 10 ya maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini. Haya yote yanatafsiri namna nchi yetu inavyofanya kazi,” alisema.