Siasa Arusha zatia aibu kwa wafadhili

File Photo

Muktasari:

Mradi huo ni wa ujenzi wa hospitali ambayo inalenga kuhudumia bure kina mama na watoto, na ambao sehemu kubwa ya gharama zake imeahidiwa na wafadhili kutoka Marekani.

Arusha. Rais John Magufuli amesema hapendi kuona mtu yeyote akimchelewesha kutekeleza ahadi zake za kuwaletea wananchi maendeleo, na wananchi wa Arusha watakuwa wakitafakari kauli hiyo baada ya kushuhudia siasa zikivuruga uzinduzi wa mradi wa maendeleo wa Sh9 bilioni.

Mradi huo ni wa ujenzi wa hospitali ambayo inalenga kuhudumia bure kina mama na watoto, na ambao sehemu kubwa ya gharama zake imeahidiwa na wafadhili kutoka Marekani.

Kuvurugika kwa hafla hiyo ni mwendelezo wa mvutano baina ya viongozi wa Chadema, hasa Godbless Lema, ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini, na Mrisho Gambo, ambaye ni mkuu wa mkoa.

Tukio la juzi, ambalo lilitokea mbele ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo na wafadhili wa ujenzi huo ambao ni taasisi ya Martenity Africa, lilitokana na Gambo kutoa historia ya mradi huo, akimtaja wakili Nyanga Mawalla kuwa ndiye aliyetoa eneo kwa ajili ya ujenzi huo, jambo ambalo Lema alilipinga akisema mteule huyo wa Rais anapotosha ukweli.