Silinde atoa malalamiko Bajeti ya Upinzani kukataliwa, wasusia bunge

Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde akitoka kwenye ukumbi wa bunge huku akiwa ameshikilia hotuba ya Bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani Bungeni kwa mwaka wa fedha 2018/2019 yenye kurasa 521 baada ya kuzuiliwa kusomwa Bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Silinde katika madai yake pia amemshutumu katibu wa Bunge.


Dodoma. Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa upande wa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde amesema Ofisi ya Bunge chini ya Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai inalivuruga Bunge.

Silinde ambaye ni Mbunge wa Momba (Chadema) ametoa kauli hiyo bungeni leo Juni 18, 2018 alipotumia kanuni ya 68 (7) kuomba mwongozo wa Spika juu ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kuzuiwa kusoma hotuba mbadala ya bajeti ya mwaka 2018/19.

Akizungumza bungeni hapo, Silinde amesema Kanuni ya 99(5) ya Bunge imevunjwa kwani upinzani waliwasilisha taarifa yao bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango lakini imeondolewa bila sababu kutolewa.

“Jumamosi saa 6.31 mchana nilimpigia mkurugenzi wa shughuli za Bunge, tukimweleza tutawasilisha hotuba ya kambi na akaniambia kwamba tuwasilishe Jumapili kabla ya saa 10 jioni,” amesema Silinde.

Silinde ameongeza kuwa, Spika Job Ndugai alitoa maelekezo kwamba taarifa za kambi ziletwe siku moja kabla na wao upinzani walifanya hivyo.

 “Jana saa 8.30 mchana, nimeleta hotuba ya kurasa 521 ili isomwe katika Bunge lako tukufu wananchi waone na nikampigia mkurugenzi wa ‘hansard’, akawa anauliza hotuba ina nakala ngapi, tukamwambia tuko ofisi ya kambi, baada ya hapo akawa hapokei simu, nikawa nampigia mkurugezi wa shughuli za Bunge hakupokea nikawa namtumia ujumbe akasema pelekeni hotuba kwa Katibu wa Bunge,” amesema

Ameongeza kuwa upinzani walitafuta watu wa kuwasaidia ili hotuba yao isikike lakini Ofisi ya Bunge imekataa.

“Tufanye nini katika hii nchi ili tueleweke, kama tumeleta mmekataa, mkurugenzi wa shughuli za Bunge amekataa,” amesema

Wakati akiendelea kuongea, Spika Ndugai akamtaka Silinde kuongea taratibu na asifoke.

Silinde akajibu: “Nimekwazika, kwa namna ofisi yako chini ya Katibu wa Bunge (Kagaigai) inavyokwamishwa na Katibu wa Bunge anaharibu Bunge, nimemwandikia barua hii wanipe sababu na hawajazisema.”

Akijibu mwongozo huo, Spika Ndugai amesema:

“Nimeshindwa kuelewa, nikawa naangalia labda ni wikiendi imekuwa ndefu labda umeamka vibaya nini, umempelekea Katibu lini na tumeanza Bunge la bajeti Aprili, hamna hotuba yoyote mliyotoa na sababu mliyotoa wanaowaandikieni hawapo sasa kumbe mmepata wa kuwaandikia na hamna aibu kusema mmeandikiwa.”?

“Mmechanga hela, mmepata wa kuwaandikieni, kwa hiyo tuonane baadaye ili kuona tutafanyaje, kwa sababu katika ‘oder paper’ haipo, haina shida hiyo.”