Thursday, January 11, 2018

Sinema ya madiwani yaendelea, waliohamia CCM sasa wafikia 21

 

By Mussa Juma, Mwananchi mjuma@mwananchi.co.tz

Arusha. Wimbi la madiwani wa Chadema kuhamia CCM limeendelea kushika kasi baada ya wengine watatu wa Halmashauri ya Longido mkoani Arusha kufuata mkondo huo.

Kujiuzulu kwa madiwani hao watatu kunafanya idadi ya waliojitoa Chadema na kujiunga CCM kufikia 21.

Kujivua uanachama na nyadhifa zao kunailazimisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuandaa uchaguzi mdogo katika kata hizo, jambo ambalo limelalamikiwa kuwa linapoteza fedha za walipa kodi.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Longido, Jumaa Mhina alithibtisha jana kujiuzulu kwa madiwani hao, akiwataja kuwa ni Jacob Silas Mollel wa Kata ya Elang’atadapash, Elias Mepukori Mbao (Kamwaga) na Diyoo Lomayani Laizer wa Olmolog.

Mhina alisema sababu za kujiuzulu madiwani hao ni kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli katika vita dhidi ya ufisadi, kuinua uchumi na pia kurejesha nidhamu kazini.

“Tayari tumepokea barua zao na tumezipeleka Tamisemi kwa ajili ya utaratibu wa kusheria ili kuwezesha kufanyika uchaguzi mdogo baada ya tume kupata taarifa,” alisema.

Madiwani hao ambao kabla ya kujiunga na Chadema walikuwa CCM, walisema walihamia chama hicho kikuu cha upinzani kutokana na walichoeleza kuwa ni kutoridhishwa na mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM ambao ulifanyika mwaka 2015.

Aliyekuwa mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole pia jana alithibitisha kuondoka kwa madiwani hao na kueleza kuwa chama hicho kinafuatilia tukio hilo.

Uamuzi wa madiwani hao kujiunga na CCM unafanya Mkoa wa Arusha pekee kuwa na jumla ya madiwani 13 wa Chadema ambao wamejiuzulu na kujiunga na chama hicho tawala tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu 2015.

-->