VIDEO: Sirro awaonya wanaobeza polisi mitandaoni

Muktasari:

Jeshi la Polisi Tanzania limeonya makundi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kubeza jitihada zilizofanywa na polisi katika uchunguzi wa tukio la kutekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’

Dar es salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limeonya makundi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kubeza jitihada zilizofanywa na polisi katika uchunguzi wa tukio la kutekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.

Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 20, 2018 na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari saa chache baada ya mfanyabiashara huyo aliyetekwa Oktoba 11 kupatikana.

Sirro amesema yeyote atakayeanzisha ugomvi na polisi hatobaki salama.

Amesema polisi wako imara na litawashughulikia wote aliodai kuwa wana dhamira ya kuvuruga utendaji wa jeshi hilo.

“Nawaomba sana wasilazimishe kujenga uadui na Polisi lakini wanafanya hivyo ili iweje na kwanini? Wametumwa na nani?" amesema.

Kabla ya kueleza hayo, Sirro alifafanua jinsi Mo Dewji alivyopatikana na kubainisha kuwa watekaji walimtupa katika viwanja vya Gymkhana na kisha kutelekeza gari.