Sitta aenda Ujerumani kwa matibabu

Samweli Sitta

Muktasari:

Septemba 19, Rais John Magufuli alimtembelea Sitta nyumbani kwake ambako alimueleza kuwa hali yake inaendelea vizuri.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta amekwenda Ujerumani kwa ajili ya matibabu ya miguu.

Mwanawe, Benjamin Sitta amesema: “Anachoumwa ni miguu. Baba yupo katika hali nzuri, yupo salama tu, achaneni na taarifa za mitandao.” Alikuwa akirejea taarifa zilizoenea kwenye mitandao kwamba baba yake yu mahututi.

Septemba 19, Rais John Magufuli alimtembelea Sitta nyumbani kwake ambako alimueleza kuwa hali yake inaendelea vizuri. Taarifa ya Ikulu ilieleza  mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa jijini kwa ajili ya matibabu bila kueleza ugonjwa unaomsumbua.

Siku moja baada ya Rais kumtembelea,  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye alikwenda kumjulia hali. Vivyo hivyo, Septemba 21 Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alimtembelea Sitta alipokuwa amelazwa katika hospitali moja jijini hapa.

Sitta ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba na waziri katika wizara mbalimbali kwa vipindi tofauti, ni miongoni mwa wanachama  zaidi ya 40 wa CCM waliochukua fomu za kugombea urais mwaka jana. Hata hivyo, baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kumuondoa, alitangaza kustaafu masuala ya siasa.