Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Msoka Rais mpya wa MAT, aahidi mambo matano

Muktasari:

  • Amesema mambo hayo matano yatajenga chama imara na kuchangia mfumo wa afya bora nchini

Dar es Salaam. Rais mpya wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Alex Msoka ameanza rasmi majukumu yake akiahidi mambo matano kwa wanachama wake, ikiwemo kuweka kipaumbele kwenye kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).

Mambo mengine ni kuimarisha mfumo wa afya nchini, kulinda na kuimarisha ustawi wa wanachama, kuifanya MAT kuwa sauti imara pamoja na kujenga umoja, uwazi na uwajibikaji ndani ya chama hicho.

Dk Msoka aliyeapishwa jana Juni 19, 2026 ataongoza chama hicho kwa miaka miwili ya 2026 hadi 2028 akichukua kijiti kutoka kwa mtangulizi wake Dk Mugisha Nkoronko ambaye amemaliza muda wake.

Mwaka 2024, Dk Msoka alichaguliwa kuwa Rais mteule wa chama hicho cha kitaaluma huku Dk Nkoronko akipokea kijiti cha urais kutoka kwa mtangulizi wake Dk Deusdedith Ndilanha.

Kulingana na taarifa iliyotolewa leo Juni 20, 2026 na MAT kupitia mitandao yake ya kijamii, Dk Msoka tayari ameapishwa kukiongoza chama hicho akiahidi mambo matano.

Rais Mstaafu wa MAT, Dk Mugisha Nkoronko (kushoto) akimpongeza Rais mpya wa Chama hicho, Dk Alex Msoka.

Kwenye eneo la magonjwa yasiyoambukiza, Dk Msoka amesema watahamasisha nguvu zaidi katika kinga, elimu ya afya na mikakati ya kupunguza mzigo wa magonjwa hayo.

"Tukiimarisha kinga, tutasaidia kupunguza gharama kubwa za matibabu na kulinda afya ya wananchi wetu kwa muda mrefu," amesema.

Ahadi nyingine, Dk Msoka amesema atalinda na kuimarisha ustawi wa wanachama wake.

"Nitahakikisha maslahi, usalama, heshima na utu wa kila daktari Tanzania vinapewa kipaumbele. Tutafanya kazi kuhakikisha mazingira ya kazi yanaboreshwa na sauti ya daktari inasikika.

"Ninaamini daktari anayethaminiwa, anayelindwa na kuheshimiwa ana uwezo mkubwa zaidi wa kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kuchangia maendeleo ya mfumo wa afya," amesema.

Pia, Dk Msoka amesema ataimarisha ushauri wa kitaaluma, maendeleo ya madaktari na uongozi.

Katika hilo amesema atajenga mifumo imara ya mafunzo endelevu na maendeleo ya taaluma kuanzia madaktari wanaoanza safari yao hadi wataalamu wenye uzoefu.

"Maarifa, uzoefu na misingi ya taaluma yetu lazima viendelee kutoka kizazi hadi kizazi ili kuandaa madaktari wenye uwezo, maadili na uongozi bora," amesema.

Ahadi nyingine ya Dk Msoka ni kuifanya MAT kuwa sauti imara katika sera za afya na kuimarisha Dira ya Afya kuelekea 2050.

"Chama cha Madaktari Tanzania kitaendelea kuwa mshirika muhimu katika uundaji wa sera za afya.

"Tutashirikiana na Serikali, taasisi na wadau mbalimbali kuhakikisha maamuzi ya afya yanazingatia ushahidi wa kisayansi, uhalisia wa huduma na mahitaji ya wananchi," amesema.

Rais mteule wa MAT, Dk Mathew Shao.

Dk Msoka amesema ataimarisha misingi ya Dira ya Afya kuelekea 2050 kwa kuhakikisha kunajengwa mfumo wa afya wenye ubunifu, teknolojia, utafiti, ubora wa huduma na viongozi wa kitabibu watakaoongoza mabadiliko ya kizazi kijacho.

Jambo la mwisho, Dk Msoka amesema atajenga umoja, uwazi na uwajibikaji ndani ya chama hicho.

Amesema MAT ni chama cha wanachama wote hivyo ataimarisha mawasiliano ya wazi, ushirikiano, uwajibikaji na umoja.

"Tutajenga chama chenye nguvu, kinacholinda taaluma ya udaktari na kuwa chachu ya maendeleo ya afya ya Tanzania. Daktari wa mwaka 2050 lazima awe mtaalamu, kiongozi, mbunifu, mtafiti na mshiriki muhimu katika maendeleo ya taifa," amesema na kuongeza:

"Safari hii ni yetu sote. Pamoja tutajenga MAT yenye nguvu, yenye sauti na yenye dira ya afya ya Tanzania ya kesho," amesema.

Kwa upande wake, Rais mteule Dk Mathew Shao amewashukuru wanachama wenzake kwa imani waliyompa akisisitiza anatambua dhamana aliyopewa ni kubwa.

"Katika nyakati ambazo sekta ya afya inaendelea kubadilika kwa kasi, jukumu letu ni kuendelea kusimamia weledi, maadili, ubora wa huduma, elimu endelevu, ustawi wa wanataaluma na taaluma, na ushahidi wa kisayansi katika kila tunachokifanya.

"Nguvu ya taaluma yetu haipo kwa mtu mmoja, bali katika umoja wetu, uwezo wetu wa kushirikiana, na kujitolea kwetu kwa wananchi tunaowahudumia," amesema Dk Shao.

Amesema anaamini madaktari wa Tanzania wana nafasi muhimu si tu katika kutibu magonjwa, bali pia katika kuchangia fikra, sera na mwelekeo wa maendeleo ya taifa kupitia afya.

Dk Shao amesema taifa lenye watu wenye afya njema lina msingi imara wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

"Ninawaomba tuendelee kushikamana, kuheshimiana na kuweka mbele maslahi ya taaluma na ya Watanzania. Hiyo ndiyo njia bora ya kuacha alama chanya kwa kizazi cha sasa na vijavyo," amesema.