Wauguzi wanavyoibeba sekta ya afya, walilia muundo mpya wa utumishi
Wauguzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili MOI, wakiwa wamewasha mishumaa kuadhimisha siku yao Mei 12 mwaka 2024. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Takwimu duniani kote zinaonesha zaidi ya asilimia 80 ya huduma kwa mgonjwa hutolewa na muuguzi kabla na baada ya mgonjwa kumuona daktari.
Dar es Salaam. Wakati wauguzi wakitajwa ndio mhimili mkuu wa utoaji huduma za afya nchini, kada hiyo bado inakabiliwa na changamoto za mazingira ya kazi, uhaba wa watumishi na muundo wa utumishi unaodaiwa kutowatambua kulingana na taaluma na majukumu yao.
Kwa mujibu wa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanana), muundo mpya wa utumishi wa kada ya uuguzi na ukunga, umekwama kwa miaka 13.
Muundo huo hautambui wauguzi wenye Stashahada ya Juu na Shahada za Uzamili, maarufu kama wauguzi bingwa, jambo linalosababisha kutokuwepo kwa utofauti wa mishahara na majukumu kulingana na kiwango cha elimu na utaalamu.
Hayo yameelezwa leo Mei 12, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mchango wa wauguzi katika mfumo wa afya unaanzia hatua ya kwanza kabisa mgonjwa anapoingia hospitalini hadi mwisho wa huduma.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema madaktari wanatambua mchango mkubwa wa wauguzi katika utoaji huduma za afya na wanaunga mkono jitihada za kuboresha mazingira yao ya kazi.
“Wauguzi ni nguzo muhimu ya huduma za afya nchini. Wao ndio wanaotekeleza mpango wa matibabu unaoelekezwa na madaktari na ndio wanaowahudumia wagonjwa wetu kila siku,” amesema.
Amesema uwekezaji zaidi unahitajika katika taaluma za ubingwa wa uuguzi ikiwamo uuguzi wa watoto, huduma za wagonjwa mahututi na huduma za upasuaji ili kuongeza ubora wa huduma za afya nchini.
Tanana yataka muundo mpya
Katika maadhimisho ya kitaifa yaliyofanyika leo mkoani Arusha, wauguzi kupitia Tanana, wametumia jukwaa hilo kuiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa muundo mpya wa utumishi wa kada ya uuguzi na ukunga uliokwama kwa miaka 13.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Regina Qwaray aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanana, Dk Ezekiel Mbao amesema muundo wa sasa wa mwaka 2009 hauendani tena na hali halisi ya taaluma hiyo.
Amesema muundo huo hautambui wauguzi wenye Stashahada ya Juu na Shahada za Uzamili, maarufu kama wauguzi bingwa, jambo linalosababisha kutokuwepo kwa utofauti wa mishahara na majukumu kulingana na kiwango cha elimu na utaalamu.
“Tunaiamini Serikali hii sikivu itatekeleza muundo huo katika mwaka wa fedha 2026/27 kama ilivyoahidiwa hapo awali,” amesema Dk Mbao.
Mbali na masuala ya mishahara, Tanana pia imetaka kufanyika kwa marekebisho ya Sera ya Afya na Sheria ya Afya ya Jamii ili wauguzi waweze kushika nafasi za juu za uongozi katika wizara na hospitali kulingana na taaluma na uzoefu wao.
Katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo: “Wauguzi Wetu, Mustakabali Wetu: Wauguzi Waliowezeshwa Huokoa Maisha,” wauguzi walitoa huduma za afya bure kwa wananchi 84,149 mkoani Arusha.
Huduma hizo zilijumuisha upimaji wa shinikizo la damu, sukari, Virusi vya Ukimwi (VVU) pamoja na uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi. Jumla ya wagonjwa 9,479 waliofanyiwa uchunguzi walipatiwa matibabu.
Maoni ya wauguzi
Muuguzi kutoka Hospitali ya Vijibweni, Rehema Nyachuma amesema zaidi ya asilimia 80 ya huduma kwa mgonjwa hutolewa na muuguzi kabla hata ya mgonjwa kumuona daktari.
Amesema katika baadhi ya vituo vya afya na zahanati, muuguzi ndiye anayebeba jukumu kubwa la utoaji huduma kutokana na uhaba wa madaktari na wataalamu wengine wa afya.
“Mama mjamzito anaweza kufika hospitalini na kuhudumiwa na muuguzi hadi kujifungua bila kumuona daktari. Muuguzi anaweza kutoa dawa, kufanya vipimo vya msingi, kutoa huduma za dharura na kuhakikisha mgonjwa anapata huduma zote muhimu,” amesema Rehema.
Amesema hata katika mazingira ambayo hakuna daktari au mfamasia, huduma nyingi zinaendelea kutolewa ikiwa wauguzi wapo kazini.
Rehema amesema jukumu la muuguzi linaendelea hata pale mgonjwa anapofariki dunia kwa kuwa, ndio wanaohusika na maandalizi ya mwisho ya mwili kabla ya kupelekwa mochwari.
Pamoja na umuhimu huo, amesema wauguzi wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa kazi unaotokana na uhaba wa watumishi katika hospitali na vituo vya afya.
“Muuguzi mmoja wakati mwingine analazimika kuhudumia maeneo mengi kwa wakati mmoja. Tunaweza kufanya kazi wiki nzima bila kupumzika kwa sababu hakuna wa kupokea zamu,” amesema.
Amesema hali hiyo huongeza msongo wa mawazo kwa wauguzi, huku wakati mwingine wakikumbana na lawama kutoka kwa wagonjwa bila kupewa nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili.
“Wakati mwingine hata ukichelewa dakika tano wagonjwa wanalalamika sana. Tunaweza kuwa tunakula huku tunaandika taarifa za wagonjwa, lakini bado wananchi hawaelewi mazingira tunayofanyia kazi,” amesema.
Ofisa Muuguzi wa Manispaa ya Ubungo, Tainoi Moringe amesema wauguzi ni asilimia 60 ya watumishi wote wa afya nchini na ndio wanaofanya zaidi ya asilimia 80 ya kazi katika sekta hiyo.
Kutokana na hali hiyo, amesema ni muhimu Serikali kuboresha mazingira yao ya kazi na kuhakikisha muundo wa utumishi wa Ofisa Muuguzi Msaidizi na Muuguzi Bingwa unaanza kutumika kama ilivyopendekezwa tangu mwaka 2013.
“Tunaomba mfumo wa utawala wa sekta ya afya utoe nafasi kwa kada zote kushiriki katika uongozi. Kwa sasa unaonekana kutawaliwa zaidi na kada ya madaktari,” amesema.
Amependekeza kuwepo kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Huduma za Afya badala ya mfumo wa sasa wa RMO na DMO pekee ili kada nyingine za afya nazo zipate uwakilishi katika uamuzi wa kisera na kiutendaji.
Fahamu Siku ya Wauguzi Duniani
Mei 12 ya kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Wauguzi na Wakunga Duniani kwa kutambua mchango mkubwa wa wauguzi katika huduma za afya.
Siku hii inamheshimu Florence Nightingale maarufu kama “Mwanamke wa Taa,” ambaye alikuwa mwanzilishi wa mageuzi ya kisasa ya uuguzi.
Florence alianza harakati zake mwaka 1854 nchini Uturuki wakati wa Vita ya Krimea alipokuta hospitali zikiwa katika hali mbaya ya uchafu na wagonjwa wengi wakifariki dunia kutokana na maambukizi.
Akiwa na wasaidizi wake 38, alisimamia usafi hospitalini na kuboresha huduma kwa wagonjwa.
Kupitia juhudi zake, taaluma ya uuguzi ilianza kuthaminiwa zaidi duniani. Florence alisisitiza umuhimu wa usafi, elimu kwa wagonjwa na uangalizi wa karibu kwa wagonjwa.
Alijulikana kama “Mwanamke wa Taa” kwa sababu alikuwa akiwatembelea wagonjwa usiku akiwa amebeba taa mkononi.
Florence Nightingale alizaliwa Mei 12, 1820 nchini Italia na baadaye kusomea uuguzi Ujerumani kabla ya kurejea Uingereza.
Pia, alianzisha Shule ya Uuguzi ya Nightingale mwaka 1860 katika Hospitali ya St. Thomas na kuandika vitabu vya uuguzi na ukunga.
Urithi wake unaendelea kuenziwa kila mwaka kupitia maadhimisho haya muhimu duniani.