Suala la Balozi wa EU, waandishi wa CPJ latua bungeni

Muktasari:

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Salome Makamba ametoa hoja ya kutaka shughuli za Bunge kuahirishwa ili kujadili suala la Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Roeland Van de Geer na waandishi wa Kamati Maalumu ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), Angela Quintal na Muthoki Mumo

Dodoma. Sakata la balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Roeland Van de Geer, wavuvi 37 wa Kenya na waandishi wa Kamati Maalumu ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) limetua ndani ya Bunge kwa mbunge kutaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili kujadili mambo hayo.

 

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Salome Makamba amesema mambo hayo ni muhimu zaidi. Makamba ametoa hoja hiyo leo Alhamisi bungeni jijini Dodoma, Novemba 8, 2018.

 

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai ameikataa hoja ya Makamba kwa madai alikuwa amechanganya mambo na kwamba hoja yake haikupata mtu wa kuiunga mkono.

 

Makamba amesimama ndani ya Bunge baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni akiomba Bunge lisitishe mambo yote kwani Tanzania inajiingiza katika doa nje ya mataifa yenye misaada na misaada ya bajeti.

 

“Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako tukufu lisitishe shughuli zake ili tujadili jambo la dharura ambalo liko mbele na ni jambo muhimu sana mheshimiwa Spika," amesema Makamba.

 

Mbunge huyo amesema ni muda muafaka kwa Serikali kutoa matamko na ufafanuzi kuhusu sakata la balozi wa EU kwani maneno yanayosemwa yanatia hofu kwa nchi katika medani za demokrasia.

 

Amesema hata suala la kukamatwa kwa wavuvi 37 wa nchi ya Kenya bado ni ukakasi kwa mahusiano.

 

"Kingine ni hili suala la waandishi wawili ambao wanazuiliwa na uhamiaji, naomba tujadili na Serikali ije na majibu ya kina kuhusu jambo hili," amesema Makamba.

 

Hata hivyo, Spika Ndugai amekataa hoja ya mbunge huyo akisema mbunge huyo alikuwa amechanganya mambo mengi bila ya kueleza moja kwa moja alitaka kitu gani.

 

Mbali na hilo, Ndugai amesema Makamba hakuwa ameungwa mkono na wabunge wengine hivyo akaamuru Bunge liendelee.