VIDEO-TRA yabaini mambo saba ukaguzi kanisani kwa Askofu Kakobe

Muktasari:

TRA ilifanya uchunguzi huo kutokana na kauli ya Askofu Kakobe aliyoitoa alipozungumza na waumini wake katika mkesha wa Krismasi mwishoni mwa mwaka jana kwamba ana fedha kuliko Serikali.

Uchunguzi uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) linaloongozwa na Askofu Zachary Kakobe umebaini mambo saba.

TRA ilifanya uchunguzi huo kutokana na kauli ya Askofu Kakobe aliyoitoa alipozungumza na waumini wake katika mkesha wa Krismasi mwishoni mwa mwaka jana kwamba ana fedha kuliko Serikali.

Baada ya kauli hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere alisema watafanya uchunguzi kubaini utajiri huo.

Askofu Kakobe aliijibu TRA kwa kusema kuwa hana wasiwasi wa kuchunguzwa utajiri wake.

Akieleza kilichobainika katika uchunguzi huo alipozungumza na waandishi wa habari jana, Kichere alisema wamebaini kuwa Askofu Kakobe hana akaunti wala fedha katika taasisi yoyote ya fedha nchini zaidi ya kuwa mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti za kanisa.

Alisema akaunti za kanisa hilo zipo katika Benki ya NBC zikiwa na zaidi ya Sh8 bilioni.

Kichere alisema fedha hizo zilitokana na sadaka, zaka na changizo zitolewazo na waumini wa kanisa hilo, hivyo kwa mujibu wa sheria hazitozwi kodi.

Pili, Kichere alisema kanisa lilikwepa kulipa kodi ya Sh20 milioni ambazo zilitokana na uwekezaji katika kampuni za kukuza mtaji na kodi hiyo imelipwa baada ya uchunguzi.

Jambo la tatu, Kichere alisema kampuni inayomilikiwa na watoto wa Askofu Kakobe ilikwepa kulipa kodi ya Sh37 milioni ambazo zimelipwa baada ya uchunguzi.

“Jumla fedha zilizolipwa baada ya uchunguzi huu ni Sh58 milioni,” alisema.

Nne, alisema kanisa hilo linatunza kiasi kikubwa cha fedha kwenye ndoo na majaba kinyume cha utaratibu wa utunzaji wa fedha.

TRA katika suala ya tano, imesema uwekaji na utoaji wa fedha nyingi benki haushirikishi vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya usalama wa fedha zenyewe na wahusika.

Sita, uchunguzi huo pia ulibaini kuwa kanisa hilo halitengenezi hesabu za mapato na matumizi jambo ambalo ni kinyume na katiba ya kanisa na sheria ya usimamizi wa fedha.

Kichere alisema hali hiyo ya kutokuwa na usimamizi wa fedha inasababisha matumizi mabaya ya fedha ikiwamo safari za nje ya nchi ambazo zimedhaminiwa na kanisa, lakini wanaosafiri ni Askofu Kakobe na familia yake.

TRA katika suala la saba imesema fedha za kanisa zinatumika kujenga nyumba ya mke wa Askofu Kakobe kwa jina lake na si kwa jina la kanisa jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu wa kanisa.

Kutokana na uchunguzi huo, Kichere alitoa wito kwa taasisi zote za dini ambazo zinajihusisha na shughuli zozote za kiuchumi kulipa kodi stahiki na kwa wakati kwa mujibu wa sheria, kanuni na utaratibu wa ulipaji kodi.

“Pia taasisi za kidini zifuate katiba zao ikiwa ni pamoja na kutengeneza hesabu za mapato na matumizi,” alisema Kichere.

“Wakati uchunguzi huo ukiendelea Januari 24, Askofu Kakobe alimuandikia barua Rais John Magufuli ya kuomba radhi kutokana na kauli yake ya kebehi pamoja na matamshi yake ya dharau kwamba ana fedha nyingi kuliko Serikali,” alisema Kichere.

Askofu Kakobe hakupatikana ili kuzungumzia taarifa hiyo ya TRA lakini mtenda kazi wa kanisa hilo, Natus Mwita alisema tangu maofisa wa TRA walipoondoka mara ya mwisho walipokwenda kanisani hapo hawakuwahi kurejea na hana fununu zozote akisema hajaona barua wala taarifa zozote kuhusu kanisa au Askofu Kakobe.

“Kuhusu kama askofu aliandika barua ya kumuomba radhi Rais Magufuli, muulizeni askofu kwa sababu mimi sijaiona wala sikushiriki kuiandika,” alisema Mwita.

Alisema wakipata taarifa hiyo ya TRA wataijadili, lakini kwa sasa bado hawajapata.