Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete yawa tegemeo Afrika Mashariki, Kati

Muktasari:

Unaweza kuhisi upo katika hospitali ya kimataifa pindi utakapoingia ndani ya jengo hilo, kutokana na mpangilio uliopo na namna shughuli zinavyoendeshwa na madaktari waliobobea katika kutoa huduma za kibingwa ambazo kwa kipindi kirefu zimekuwa zikitarajiwa kutolewa katika nchi za mbali.

Dar es Salaam. Unapolifikia jengo la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kitu cha kwanza utakachokutana nacho ni unadhifu, ulinzi madhubuti na miundombinu wezeshi kwa kila mgonjwa anayefika kutibiwa.

Unaweza kuhisi upo katika hospitali ya kimataifa pindi utakapoingia ndani ya jengo hilo, kutokana na mpangilio uliopo na namna shughuli zinavyoendeshwa na madaktari waliobobea katika kutoa huduma za kibingwa ambazo kwa kipindi kirefu zimekuwa zikitarajiwa kutolewa katika nchi za mbali.

Mkurugenzi wa Tiba wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema taasisi hiyo hivi sasa imejichukulia umaarufu Afrika Mashariki na Kati kwa ubingwa wa kutibu magonjwa ya moyo kwa njia ya upasuaji wa kufungua vifua na ule wa kutumia mishipa ya damu ili kuzibua iliyoziba kwa kutumia mtambo maalumu wa Catherization Laboratory (Cath Lab) ambao uliigharimu Serikali kiasi cha Sh4 bilioni kuununua mwaka 2013.

Aliutaja mtambo huo, kuwa ni kitendea kazi ambacho kimekuwa kikirahisisha matibabu kwa muda mfupi na kwa wagonjwa wengi.

Dk Kisenge ambaye pia ni bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya moyo alisema mtambo huo ambao kwa Afrika Mashariki na kati upo nchini pekee, una uwezo wa kuziba matundu kwenye moyo pamoja na kupima presha ya moyo.

Alizitaja kazi zingine za mtambo huo kuwa ni kuwasaidia madaktari kupata maelezo mazuri kabla hawajamfanyia mgonjwa upasuaji mkubwa wa moyo, kwani huchukua picha ambayo itamsaidia anayefanya kazi hiyo kujua namna ya kuitimiza kikamilifu.

“Pia mtambo huu unafanya kazi ya kuzibua mishipa ya moyo iliyoziba, wakati mwingine inaweza kutibu moja kwa moja au kugundua tatizo la mgonjwa husika,” alisema Dk Kisenge.

Alisema kutokana na mafanikio hayo, taasisi hiyo imeokoa fedha nyingi ambazo Serikali ilikuwa ikizitumia kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

“Tumeokoa maisha ya wagonjwa wengi, lakini vilevile tumeweza kuokoa fedha nyingi kwa sababu sasa wagonjwa wengi waliopaswa kupelekwa India kwa matatizo ya moyo, wanatibiwa katika taasisi yetu hii ya JKCI,” alisema.

Alisema kabla ya taasisi hiyo kuanza kutoa huduma, Watanzania wengi wenye shida ya moyo walikuwa wanapelekwa nje kwa ajili ya matibabu idadi ambayo imepungua kwa asilimia 80.

Alisema ni kutokana na mafanikio hayo, Taasisi hiyo imekuwa kituo cha kufundishia masuala ya upasuaji wa moyo Afrika.

“Tunapokea wanafunzi wanaotoka vyuo mbalimbali vya Afrika, kituo hiki kimeshafikiriwa kuwa ndiyo chuo cha matibabu ya moyo, JKCI itatoa mafunzo kwa wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali Afrika Mashariki na Kati. Hapa ndipo madaktari wa upasuaji wa moyo watakuja kupata utaalamu wa upasuaji,” alisema Dk Kisenge.

Alisema taasisi hiyo pia inacho kipimo kinachojulikana kwa jina la Fetal Echo, maalumu cha kuwapima wajawazito ili kuangalia endapo mtoto aliyeko tumboni analo tatizo la moyo.

“Tunahamasisha kina mama wajawazito waje kupima kwani itasaidia kujua mapema endapo mtoto ana tundu la moyo na hivyo kabla hajazaliwa tunakuwa tumeshaandaa matibabu yake,” alisema.

Hata hivyo, alisema mwamko ni mdogo na akawataka wajawazito kujitokeza ili kuepuka kujifungua watoto wenye matatizo ya moyo.

“Kipimo hiki ni kama kilivyo kile cha Ultra Sound, hakina mionzi wala madhara yoyote kwa mjamzito endapo atapimwa, tunaendelea kuwaelimisha wajawazito waje wafanyiwe kipimo hiki kwa ajili ya usalama na afya kwa watoto wanaotarajia kujifungua,” alisema.

Aidha, Dk Kisenge alisema takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watoto milioni moja wanaozaliwa nchini kwa mwaka, 100,000 hukutwa na matatizo ya moyo.

Alisema tatizo la magonjwa ya moyo ni kubwa kwa watoto kiasi cha kwamba wodi zilizopo katika taasisi hiyo hazitoshelezi kwani zina vitanda 103 na kati ya hivyo, vya watoto ni 20 tu, hivyo hulazimika kuwalaza kwenye wodi za watu wazima.

“Kama JKCI itaongezewa jengo jingine kwa ajili ya watoto tu, wawe na wodi zao, vyumba vyao vya upasuaji, mtambo wao wa Cath lab pamoja na vyumba vya wagonjwa mahututi, huduma kwa watoto zitakuwa zimeboreka,” alisema Dk Kisenge.

 

Madaktari waliopo

Akizungumzia wataalamu waliopo katika taaasisi hiyo, Dk Kisenge alisema inayo timu katika kila nyanja zinazohusiana na masuala ya magonjwa ya moyo wakiwamo madaktari bingwa waliobobea.

“Tunao wataalamu wengi katika maeneo yote, ingawa bado hatuwezi kusema kuwa wanatosha, lakini tunao wengi wanaotambulika katika viwango vya kimataifa, naweza kusema ni hospitali ambayo imejitosheleza upande wa madaktari na watumishi wake,” alisema.

 

Wagonjwa kutoka nje

Dk Kisenge alisema kwa sasa taasisi hiyo inapokea wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali hasa nchi za Afrika Mashariki na Kati kama vile Uganda, Kenya, Visiwa vya Comoro, DRC Congo, Rwanda na Burundi.

Kadhalika, Dk Kasenge alisema mafanikio waliyoyapata ni pamoja na kusambaza huduma hiyo nje ya nchi. Alisema mwishoni mwa mwaka jana, timu ya madaktari bingwa wa moyo kutoka taasisi hiyo ilikwenda Rwanda kwa ajili ya upimaji na upasuaji wagonjwa wa moyo.

“Timu ya madaktari wanne wa upasuaji watoto na daktari wa tiba ya watoto na wawili wa usingizi kutoka katika taasisi yetu ilikwenda Rwanda kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa waliokuwa wakisumbuliwa na matatizo hayo… hiki ni miongoni mwa vitu ambavyo tunavyojivunia,” alisema.

Aliongeza kuwa wanao mpango wa kuipeleka huduma hiyo katika nchi za Afrika Kusini na visiwa vya Comoro.

“Mpango wetu ni kuisambaza huduma hii dunia nzima, lakini kwa hivi sasa tunajiandaa kwenda Comoro, tunataka kwenda kutibu katika nchi zote za Afrika kama ambavyo wataalamu wanatoka nje na kuja kutoa huduma hapa, vivyo hivyo na sisi tunataka kutoka nje,” alisema.

 

Malengo ya JKCI

Akizungumzia malengo ya taasisi hiyo, Dk Kisenge alisema: “Mwaka huu tunataraji kufanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa wagonjwa 1,200 kwani mwaka jana tulifanya kwa wagonjwa 623.”

Alisema hata hivyo, wanajivunia kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wametibiwa na wazawa, huku asilimia 30 pekee ndiyo waliotibiwa na madaktari wanaotoka nje.

“Baada ya kupata ujuzi wazawa wanafanya kazi zaidi…, hivi sasa tunaye mtaalamu mmoja tu wa upasuaji wa moyo kutoka nje ya nchi, mmoja wa tiba ya moyo na mwingine wa ICU jumla ni watatu, lakini wazawa ni wengi zaidi.

 

Mafanikio

“Tumeokoa fedha nyingi zilizokuwa zitumike kupeleka wagonjwa nje kwa gharama kubwa, tumewajengea imani Watanzania ambao walikuwa wakisumbuliwa na matatizo ya moyo, tumeokoa maisha ya Watanzania wengi ambao zamani walipokuwa wakifariki kutokana na matatizo haya tulikuwa tunasema ‘ni kazi ya Mungu,’ lakini kwa sasa wengi wanapata tiba na msaada wa kitaalamu,” alisema.