Tanesco Mbeya wataja sababu umeme kukatika

Muktasari:

Sababu hizo ni chakavu wa transfoma, nguzo na nyaya za kusambaza nishati hiyo

 Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mbeya limeeleza kuwa sababu za kukatika kwa nishati hiyo  mara kwa mara mjini humo ni uchakavu wa transfoma, nguzo na nyaya za kusambaza nishati hiyo.

Meneja wa Tanesco, Mkoa wa Mbeya,  mhandisi Benedict Bahati amesema hayo leo Machi 7, 2018  wakati wa ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa pamoja na kubadilisha nguzo chakavu 420 na kuboresha transfoma 30  jijini hapa.

“Tumeamua kufanya maboresho makubwa katika huduma zetu kutokana na changamoto za kukatika kwa umeme mara kwa mara jambo lililokuwa likisababishwa na ubovu wa miundombinu.

“Tumefanya maboresho ya kuondoa nyaya chakavu katika maeneo mbalimbali katikati ya jiji na kufanya usafi katika maeneo ya msongo mkubwa wa umeme,” Bahati. Ametaja maeneo  yalikuwa na changamoto  hiyo  kuwa ni  Mbalizi, Gombe uyole, Simike, Ilemi, Juhudi na Mbalizi mageuzi ndani ya Jiji la Mbeya.

Amesema katika miradi wa Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (Rea) awamu ya pili wamefanikiwa kusambaza umeme katika vijiji 194, kati ya hivyo 164 vitanufaika awamu ya tatu ambayo inaendelea kwa sasa.

Ofisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Mbeya, Kembe Sabini amesema: “changamoto kubwa ni wananchi kuhujumu miundombinu ya shirika  hususani nyaya za umeme na kujiunganishia umeme  kinyume cha sheria.”

Sabini amesema changamoto hizo zinaathiri utendaji wa shirika jambo linalochangia wananchi kukosa huduma na kupelekea uzalishaji kupungua kwa kiasi kikubwa.