Tanzania yailalamikia Kenya kukiuka taratibu za biashara Jumuiya ya Afrika Mashariki

Muktasari:

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo (Jumatano) na Katibu Mkuu, Biashara na Uwekezaji, Adolph Mkenda imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya Kenya kupiga marufuku uingizwaji wa gesi ya kupikia kutoka Tanzania na kutoza kodi unga wa ngano unaotoka nchini.

Dar es Salaam. Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, imepeleka rasmi malalamiko yake nchini Kenya kwa kukiuka taratibu za biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo (Jumatano) na Katibu Mkuu, Biashara na Uwekezaji, Adolph Mkenda imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya Kenya kupiga marufuku uingizwaji wa gesi ya kupikia kutoka Tanzania na kutoza kodi unga wa ngano unaotoka nchini.

“Walizuia gesi hiyo na kusema kuwa gesi itakayoruhusiwa kuingia Kenya ni ile itakayokuwa imepitia Bandari ya Mombasa peke yake,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema kuwa baada ya kusoma taarifa hizi Serikali ya Tanzania iliwasiliana na Serikali ya Kenya ili kupata maelezo kuhusu hatua hii ambayo ni kinyume cha taratibu za kibiashara katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa Mei 18 mwaka huu, Serikali ya Kenya ilitekeleza uamuzi wake kwa kuzuia shehena ya gesi isiingie Kenya kutokea Tanzania.

“Hatua hii ina athari kubwa kwa wafanyabiashara wa gesi ya kupikia hapa nchini pamoja na watu wote ambao ajira zao zinategemea biashara hii,” imesema taarifa hiyo.

Imesema suala hilo lilijadiliwa kwa kina katika kikao cha Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kilichofanyika Juni, 2017 na kufanyiwa maamuzi.

Imesema Serikali ya Kenya ilikubali kuondoa katazo la uingizaji wa gesi kupitia Tanzania mara moja na makubaliano haya yaliingizwa kwenye kumbukumbu za mkutano ambazo ziliafikiwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya kwa kuweka sahihi.

Pia imeeleza kuwa pamoja na makubaliano hayo, Kenya imeendelea kuzuia gesi isiingie nchini mwao kutokea Tanzania. Serikali ya Tanzania

imewasilisha rasmi malalamiko yake Kenya kuhusu suala hili.