UN yazitaka nchi kuwekeza katika rasilimali watu

Dar es Salaam. Mkurugenzi mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Alvaro Rodriguez amesema ili nchi zote duniani zitatue changamoto zake ni muhimu wananchi na viongozi wao kuwa na utashi wa kuwekeza katika rasilimali watu.

Rodriguez amesema hayo leo Machi 17 wakati alipotembelea maonyesho ya picha zinazohamasisha utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia (SDGs), yaliyoandaliwa na kampuni ya Sahara Ventures na kufanyika katika makumbusho ya taifa jijini hapa.

"Kumaliza umasikini sasa si suala linalohitaji utaalamu bali utashi wa watu na utashi wa kisiasa  ili kila mmoja ajue namna ya kukabiliana na changamoto zinazomkabili," amesema Rodriguez.

Amesema jambo hili si la nchi zinazoendelea tu bali hata zile zilizoendelea kwa kuwa kila siku kuna changamoto mpya huibuka hususani za mabadiliko ya tabia ya nchi ambazo haziwezi kuzuilika bali kuzikabili.

"Kama tunaweza kuwekeza watu wakaeda mwezini tunashindwa nini kuwekeza kutoa elimu bora kwa vijana wetu. Tayari tunajua kuzalisha chakula cha kutosha, kupata maji hata kama yapo umbali gani ardhini na kuyatibu yale yasiyofaa," amesema.

Amesema hali ya sasa ni tofauti na miongo kadhaa iliyopita ambapo dunia ilikuwa inahofia ongezeko la watu na changamoto za baadaye lakini sasa nyingi zinaweza kutatuliwa kikubwa uwekezaji wa kutosha kwa watu.

Kuhusu maonyesho hayo Rodriguez amesema UN miaka yote imekuwa ikihamasisha kueleweka kwa malengo hayo kupitia nyaraka mbalimbali lakini huenda hata nyaraka hizo zimekuwa hazieleweki kwa watu kama ambavyo picha zinaweza kueleweka.