Mudavadi, Odinga watofautiana uchaguzi mpya

Muktasari:

  • Mudavadi, aliyekuwa mkuu wa kampeni za mgombea urais wa upinzani Odinga mwaka jana, anahimiza muungano huo badala yake ujikite kuhakikisha uchaguzi mkuu wa 2022, ambao kwa makubaliano ndani ya Nasa Odinga hatapaswa kuwania tena, unakuwa huru na wa haki.
  • "Kuna wale ambao wanaweza kutaka kufanya kile kinachojulikana kuwa ni maarufu, lakini pia kuna wale ambao wana ujasiri wakati mwingine kuwaambia watu kuwa, hiyo si njia sahihi," alisema Mudavadi.
  • "Nimewauliza wabunge wetu kama wametenga fedha kwa ajili ya uchaguzi mpya wa urais. Walisema hapana. Masuala kama haya, kwa maoni yangu, yanahitaji fedha kwa asilimia 90 kutoka kwa wananchi wenyewe na kwamba hiyo ni kupitia bajeti,” alisema Mudavadi.

Mmoja wa viongozi wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) Musalia Mudavadi ametoa kauli inayotofautiana na msimamo wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga juu ya wito wa kufanyika uchaguzi mkuu wa tatu Agosti.

Mudavadi, aliyekuwa mkuu wa kampeni za mgombea urais wa upinzani Odinga mwaka jana, anahimiza muungano huo badala yake ujikite kuhakikisha uchaguzi mkuu wa 2022, ambao kwa makubaliano ndani ya Nasa, Odinga hatapaswa kuwania tena, unakuwa huru na wa haki.

Mkanganyiko huo umekuja wakati ambao tofauti ndani ya muungano huo zinazidi kukua, tofauti ambazo zinajumuisha vita vya kiitikadi miongoni mwa wapangaji mikakati ya kushinikiza kupinga, pamoja na msukumo wa mwisho wa mikusanyiko ambayo inapendekezwa kamati tendaji, kushinikiza kuanzishwa marekebisho ya mahakama na polisi na kuimarisha ugatuzi.

Katika mahojiano na televisheni ya NTV Jumatano, naibu waziri mkuu huyo wa zamani alisema hakuna mfumo wa kisheria na kifedha ili kuwezesha nchi kufanya uchaguzi mpya, wa tatu ndani ya mwaka katika Kenya iliyokumbwa na mgogoro wa uchaguzi wa muda mrefu huku mmoja ukifutwa na mwingine ukisusiwa na Nasa.

"Kuna wale ambao wanaweza kutaka kufanya kile kinachojulikana kuwa ni maarufu, lakini pia kuna wale ambao wana ujasiri wakati mwingine kuwaambia watu kuwa, hiyo si njia sahihi," alisema Mudavadi.

Wiki mbili zilizopita, Odinga alizungumza na  Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na kusema kwamba muungano wao utashinikiza ifanyike duru ya tatu ya uchaguzi.

Mahojiano hayo yalifanyika siku kadhaa baada ya Odinga kula 'kiapo' kama rais wa watu katika sherehe ambazo Mudavadi pamoja na vinara wengine Kalonzo Musyoka na Moses Wetang'ula hawakuhudhuria.

Mudavadi alisema upande wake ndani ya muungano huo haukoa tayari kwa kipindi kingine cha uchaguzi.

"Nimewauliza wabunge wetu kama wametenga fedha kwa uchaguzi mpya wa urais. Walisema hapana. Masuala kama haya, kwa maoni yangu, yanahitaji fedha kwa asilimia 90 kutoka kwa wananchi wenyewe na kwamba hiyo ni kupitia bajeti,” alisema Mudavadi.

Mapendekezo ya mabadiliko kutoka Agosti 2018 hadi 2022 yanakuja yakiwa yamejaa hofu miongoni mwa wakuu wa Nasa kuwa Odinga anaweza kugombea tena, na yameongezeka baada ya 'kiapo' huku wafuasi wake wenye msimamo mkali wakimwambia asiwaunge mkono yeyote kati ya wakuu wenzake kwa sababu walimwangusha Uhuru Park.

Mudavadi, ambaye Jumapili aliidhinishwa na wazee wa Luhya kuwania mbio za urais za 2022, tukio hilo lilikosolewa baadaye na Wetang'ula kwamba halikuwa na uwakilishi, akisema Nasa inapaswa badala yake kushinikiza uwazi katika namna ambayo kila kura iwe na maana kabla ya uchaguzi 2022.

Alhamisi, Odinga aliongoza kikao cha chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM), ambacho kimeamua kujipanga upya kivyake.