Ukawa sasa kurejea bungeni

Muktasari:

  • Wabunge hao wamesema uamuzi wao unatokana na kutii wito wa viongozi wa dini na hekima za Spika Job Ndugai aliyeonyesha utayari wa kushughulikia madai yao.
  • Katika mkutano wa Bunge la Bajeti lililohitimishwa Juni 30, wabunge wa Ukawa, inayoundwa na vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, NLD na CUF walikuwa wakitoka ukumbini kila wakati Dk Tulia alipoongoza vikao, wakidai kuwa hawama imani naye kwa kuwa anawabagua na kukandamiza demokrasia ndani ya chombo hicho.

Dar/Mikoani. Baada ya siku 32 za kususia vikao vinavyoendeshwa na Naibu Spika Tulia Ackson, wabunge kutoka vyama vinavyounda Ukawa wameamua kurejea bungeni na kiongozi wao amesema mapambano ya kupinga ukandamizwaji na matumizi mabaya ya madaraka yatahamia kwenye chombo hicho.

Wabunge hao wamesema uamuzi wao unatokana na kutii wito wa viongozi wa dini na hekima za Spika Job Ndugai aliyeonyesha utayari wa kushughulikia madai yao.

Katika mkutano wa Bunge la Bajeti lililohitimishwa Juni 30, wabunge wa Ukawa, inayoundwa na vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, NLD na CUF walikuwa wakitoka ukumbini kila wakati Dk Tulia alipoongoza vikao, wakidai kuwa hawama imani naye kwa kuwa anawabagua na kukandamiza demokrasia ndani ya chombo hicho.

Na kutokana na Spika Ndugai kuwa nchini India ambako alikwenda kuchunguzwa afya yake, Dk Tulia ameongoza karibu vikao vyote vya nyakati za asubuhi na jioni na hivyo wabunge hao wa upinzani kuwa wanaingia ukumbini asubuhi na baada ya sala kusomwa wote kutoka nje kuanzia Mei 31 hadi Bunge lilipoahirishwa Juni 30.

Wabunge hao wameapa kuwa hawangeshiriki vikao vyote vinavyoongozwa na Dk Tulia hadi hapo madai yao yatakapopatiwa ufumbuzi, lakini baada ya kurejea kutoka India, Spika alieleza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni kuwa yuko tayari kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia ambaye pia ni mbunge wa Vunjo na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, amesema kamati ya uongozi ya kambi ya upinzani imekutana na kukubaliana kusikiliza wito wa viongozi wa dini pamoja na hekima zilizoonyeshwa na Spika Ndugai.

“Tangu mwanzo tulitaka maridhiano, ambayo ni jambo muhimu. Hatuna ugomvi na Bunge, tulikuwa na ugomvi na kiti cha Spika hasa Naibu Spika. Tulikaa na viongozi wa dini tarehe 24 (Agosti) na tumekubali ombi lao. Tunarudi,”amesema Mbatia.

Amesema kauli ya Ndugai ni ya hekima na ya kiongozi ambaye amekomaa hiyo kwa kuwa hawana mgogoro na Bunge bali Naibu Spika, wamekaa wakaona inafaa kurejea bungeni wakati chombo hicho kitakapoanza Mkutano wa Nne ambao utadumu kwa takribani wiki mbili.

Kauli hiyo ya Mbatia iliungwa mkono na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetangaza kuwa wabunge wanaotokana na Ukawa watarejea bungeni rasmi kuanzia leo kuitikia mwito wa viongozi wa dini na wazee waliowaomba kufanya hivyo.

“Mapambano dhidi ya ukandamizani na matumizi mabaya ya madaraka kukandamiza upinzani tunayoyaendesha nje sasa yanarejea rasmi bungeni,” alisema Mbowe akiwataka wabunge wote wa kambi ya upinzani kuhudhuria bungeni.

Wapinzani wanaingia bungeni  wakiwa pungufu ya wabunge watano ambao wanaendelea kutumikia adhabu walizopewa katika mkutano uliopita.

Ukawa walianza kususia vikao hivyo Mei 31 baada ya kutolewa bungeni kwa madai ya kufanya vurugu wakati walipokuwa wakishinikiza chombo hicho kuahirisha shughuli zake na kujadili suala la wanafunzi 7,802 waliotimuliwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kutokana na walimu wao kugoma wakidai malipo yao.

Hoja hiyo ilianzishwa na mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia Mei 30, lakini ilizimwa kutokana na kukosea kanuni na baadaye kudakwa na mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nasari aliyenukuu vizuri kanuni.

Lakini Naibu Spika alikataa suala hilo kujadiliwa na ndipo Ukawa walipoanza kupiga kelele hadi kiongozi huyo wa Bunge alipoamuru watolewe nje.

Baadaye wabunge hao walikutana na kuazimia kususia vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia.

Baada ya matukio hao, wapinzani walitaka kufanya mikutano kuishtaki Serikali kwa wananchi kuwa inakandamiza demokrasia, lakini Jeshi la Polisi likapiga marufuku na baadaye kufuatiwa na tamko la Rais John Magufuli, lililosababisha Chadema kutangaza operesheni iliyoitwa Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ambayo pia ilipigwa marufuku.

Marufuku hiyo ilikifanya chama hicho kutangaza maandamano na mikutano nchi nzima kushinikiza kuheshimiwa kwa Katiba na demokrasia, matukio ambayo yangefanyika kuanzia Septemba Mosi, lakini viongozi wa dini walikutana nao na Chadema ikaamua kuahirisha shughuli hiyo siku moja kabla