Tuesday, February 13, 2018

Upungufu wa mbolea unavyowapasua kichwa wakulima, mawakala Njombe

 

By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Kufuatia Mfumo wa Serikali wa ununuzi na usambazaji wa mbolea (BPS), malalamiko ya wadau zikiwamo kampuni kubwa za ununuzi na usambazaji pamoja na wakulima, wanataka Serikali iwashirikishe kikamilifu.

Wakizungumza na hivi karibuni, baadhi ya mawakala wa mbolea mjini Makambako mkoani Njombe, wameeleza kusikitishwa na mfumo huo huku wakitaka kushirikishwa zaidi na Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa mbolea.

Mwenyekiti wa Agro Dealers katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, Absalom Magoma anasema kumekuwa na upungufu wa mbolea ya kukuzia (Urea). “Hali ya mbolea ni shida kwa sasa, urea haipatikani hapa Makambako, ikipatikana ni kidogo. Tulijaribu kuagiza kutoka Kampuni ya Premium Agro Chem wakatupa masharti lazima tuchukue SA, CAN na DAP kwa pamoja, lakini sisi mahitaji yetu ni Urea kwa ajili ya kukuzia mimea,” anasema Magoma.

Anasema japo hapingani na mfumo wa uagizwaji mbolea na mfumo elekezi, lakini umekuwa chanzo cha upungufu. huo. “Mbolea ilifika tangu Novemba, mwaka jana, lakini ilikuwa chache. Agro Dealer ndiye anayechukua kutoka kwenye kampuni na kumsambazia mkulima.

Lakini uwezekano wa kuifikisha kwa mkulima kwa bei hiyo unashindikana kwa sababu ya umbali, matokeo yake sisi ndiyo tunaathirika,” anasema na kuongeza: “Mfano, mkulima anayetoka vijiji vya Lupembe au Mtanga, atalazimika kulipa nauli yake na ya kubebea mzigo kwenda na kurudi, mkulima anaweza kutumia nauli ya Sh10,000 kufuata mfuko mmoja tu.”

Akizungumzia zaidi bei elekezi, Magoma anasema bei hizo zimepangwa kwa maeneo ya mijini tu, mawakala wanaopeleka vijijini hawafaidiki nazo.

“Ningeishauri Serikali itutambue mawakala na itupangie bei zetu ili tuichukue mbolea na kumpelekea mkulima. Tatizo mfumo wa bei elekezi haujamtambua Agro Dealer (wakala),” anasema.

Akiufananisha mfumo wa sasa na ule wa mbolea ya ruzuku, Magoma anasema ulikuwa shirikishi hadi ngazi ya chini.

“Wakati wa Rais Jakaya Kikwete kulikuwa na mfumo wa mbolea ya ruzuku, lakini Serikali ya sasa imekuja na mfumo wa pamoja wa kununua mbolea, tatizo sisi Agro Dealers tumetengwa,” anasema Magoma.

Katibu wa mawakala hao wa Makambako, Mwema Olafu anakosoa mfumo wa bei elekezi na mfumo wa kuagiza mbolea kwa pamoja akisema umeathiri maeneo yenye wakulima wengi.

“Tatizo lilianza baada ya Serikali kutangaza bei elekezi, baadhi ya kampuni zilificha mbolea. Nina uhakika kwa sababu ukiagiza kiasi kikubwa cha mbolea wanakwambia labda uchukue mifuko 20 au 50 tu, wanataka waiweke mbolea ile ibaki ili baadaye waiuze kwa bei kubwa,” anadai Olafu.

Akieleza jinsi uagizwaji wa mbolea ya pamoja ulivyoathri, Olafu anasema kampuni mbili za OCP na Premium Agro Chem zilizopewa zabuni ya kuagiza mbolea zimeelemewa.

“Tangu zimechaguliwa kampuni hizo ndiyo hapo uhaba ulipoanza, kwa sababu ni kampuni mbili tu zinaagiza mbolea kuhudumia nchi kubwa yenye wakulima wengi. Hilo ni kosa kwa sababu kampuni hizo zimezidiwa,” anasema na kuongeza: “Ni bora wangeruhusu kila kampuni ilete mbolea halafu Serikali isimamie bei, bidhaa isingekuwa hadimu. Hapa Makambako ndiyo mjini, kama mbolea haipo usitegemee vijijini itapatikana. Halafu tatizo haliko hapa tu, hata ukienda Njombe, Mbeya na kwingineko mbolea haipatikani.”

Mweka hazina wa umoja huo, James Mundele maarufu ‘Siasa’, anaunga mkono hoja za Olafu akidai wazabuni walioruhusiwa kuingiza mbolea hizo wameshazidiwa.

“Ukiagiza mbolea wale wasafirishaji wanasema kuna mrundikano mkubwa wa magari kwenye kampuni zenye zabuni, hivyo wanaongeza bei ya usafirishaji bila kujali bei elekezi.

“Jambo la pili ni kukosekana kwa Urea inayohitajika zaidi. Unapolipia tani 33 ambayo ina mifuko 660, kampuni inakutaka uchukue mifuko 150 tu,” anasema. Anasema yeye akiwa mhasibu, ndiye anayethibisha fedha za kununua mbolea, lakini kila akiagiza kwa mawakala wakubwa anapunguziwa idadi ya mifuko wanayohitaji.

“Wiki iliyokwisha tulipoagiza walisema tuchukue mifuko 200 ya Urea, wiki hii wamesema nibadilishe tuchukue 150, tulipoagiza mara ya mwisho tukaona haina maana, kwa sababu mbolea kama SA, DAP na CAN zipo za kutosha na hakuna pa kuziweka, japo tunalazimishwa kuzinunua,” anasema.

“Awali, mbolea ilikuwa ikipatikana kwenye kampuni nyingine zisizo na zabuni. Kuna wakati Mohamed Enterprises walikuwa wakiuza mfuko mmoja wa Urea Sh 40,100 yaani imezidi Sh99 kwenye bei elekezi. Sasa mtu unapakia mifuko 200 unashusha kwenye duka lako, hapo utauza shilingi ngapi kwa gharama hizo?” Anahoji na kuongeza:

“Tuliwaelekeza halmashauri ya mji ili tuuze walau Sh42,000 nao wakasema watalipeleka ngazi ya mkoa. Sasa wamerudi wanasema bei haiwezi kupanda, tuuze kwa ile ya awali Sh40,001.”

Wakulima wanalizungumziaje hilo?

Kuonyesha adha hiyo, baadhi ya wakulima waliozungumza na gazeti hili katika vijiji vya Malombwe na Ikwete wanasema wameamua kutumia mbolea ya samadi baada ya kukosekana Urea.

Anthony Ngelula, mkulima wa Kijiji cha Malombwe anasema kwa kiasi kikubwa amelazimika kutumia mboji na samadi kwenye shamba lake la ekari nne japo mbolea hizo huchelewa kutoa matokeo. “Hapa nalima mahindi, nyanya na maharagwe. Upatikanaji mbolea ni mgumu ndiyo maana kwa kiasi kikubwa nimetumia samadi na mboji,” anasema.

Josephine Mfingwa mkulima wa kijiji hicho, anasema eneo kubwa la shamba lake limeathirika kwa mahindi kubadilika rangi na kuwa ya kahawia kwa kukosa mbolea.

Uchunguzi mdogo uliofanyika kijijini hapo, ulionyesha baadhi ya wafanyabiashara huuza mbolea kwa kuipima kwa kilo, jambo lililokatazwa na Serikali.

Mfano duka moja maeneo ya Ikwete lilikutwa likiuza mbolea kwa kutumia kipimo cha lita moja kwa Sh1,500.

Mmoja wa wahudumu wa duka la pembejeo la Kampuni ya Premium Agro Chem la mjini Njombe, Emmy Ayoub anakiri kulemewa na wateja wa mbolea kwa kuwa kampuni hiyo ndiyo msambazaji pekee wa mbolea za bei elekezi.

Anasema Desemba walileta tani 53 za Urea na tani 33 za DAP, Januari wakaleta tani 307 za Urea na kuna tani 81 zilikuwa njiani kutoka Dar es Salaam.

“Kampuni yetu haina magari ya kusafirisha mbolea, yaliyopo yanatumika Dar tu, hivyo tunakodisha magari ambayo pia ni shida wasafirishaji ni wengi tunanyang’anyana,” anasema.

Gazeti hili lilishuhudia msururu wa wakulima kutoka sehemu mbali za mkoa huo wakinunua mbolea katika duka hilo lililokuwa likiuza kwa bei elekezi ya Sh40,000 kwa mfuko wa kilo 50. Hata hivyo, baadhi ya maduka Mjini Njombe yalionekana yakiuza mbolea ya Urea kwa Sh50,000 kwa mfuko wa kilo 50.

Upatikanaji wa mbolea Njombe

Akieleza hali ya upatikanaji mbolea mkoani humo, Kaimu Katibu Tawala msaidizi upande wa uchumi na uzalishaji, Dk George Katemba amekiri kuwapo upungufu wa mbolea akisema ulitokana na kuchelewa kwa meli bandarini Dar es Salaam. “Tangu tumeanza msimu, mbolea ya DAP haikuwa na shida, watu walipata muda wote, lakini mbolea ya kukuzia, ambayo kwa sasa inahitajika sana, kulikuwa na upungufu kwa siku tatu nne na ulitokana na kuchelewa kwa meli,” anasema Dk Katemba.

Anasema kwa wastani mkoa huo unapata tani 20 hadi 28 kwa siku.

Kuhusu bei ya mbolea, Dk Katemba anasema wamezingatia maelekezo ya Wizara ya Kilimo ya kuongeza bei kwa maeneo ya mbali, wamewapangia bei ya kati ya Sh42,000 hadi 45,000 wakulima wa maeneo ya Ludewa na Makete.

Akifafanua zaidi, Ofisa Kilimo mkoani humo, Uisso Joel anasema upatikanaji wa mbolea ni wa kusuasua kwa sababu hata iliyoletwa haitoshi. “Hadi jana na leo (wiki mbili zilizopita), ni tani 80 tu zimeletwa hapa Njombe na kule Makambako wameshusha tani 66 za Urea. Bado mahitaji ni makubwa,” anasema.

Anasema kwa makadirio ya jumla, mkoa huo hutumia zaidi ya tani 70,000 za mbolea. Urea tani 25,000 na DAP tani 50,000. “Hata hivyo si wakulima wote wanaotumia mbolea kwa sababu mazao makuu yanayolimwa mkoa huu ni mahindi na viazi mviringo. Kwa wastani tunatumia tani 35,000 za mbolea kwenye mazao hayo makuu,” anasema Joel.

Kuhusu mfumo wa BPS kwa mkoa huo, Joel anasema una mafanikio na changamoto zake. “Mfumo huu ni mzuri kwa sababu unaondoa urasimu ukilinganisha na mfumo ule wa ruzuku. Halafu bei elekezi imewezesha kuokoa zaidi ya Sh5,000 kwa mfuko wa kilo 50 tofauti na awali. Vilevile umesaidia kudhibiti ubora wa mbolea kwa sababu wengine walikuwa wakiifungua mifuko na kuweka mbolea tofauti,” anasema na kuongeza:

“Tatizo la mfumo ni kuchelewa kwa mbolea na inapofika inakuwa haitoshi.”

Akitaja sababu za baadhi ya mbolea kuuzwa Sh50,000 kwa mfuko wa kilo 50, Joel anasema mbolea hiyo japo ni Urea lakini ni aina ya Amidas ambayo haipo kwenye bei elekezi ya Serikali, iliyopo kwenye bei elekezi ni aina ya Amigran.


-->