Ushindi mkubwa katika rasilimali madini

Rais John Magufuli akishuhudia mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya Barrick Gold, Profesa John Thornton (wa pili kulia) na waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi (wa pili kushoto) wakitia saini makubaliano ya uwekezaji wa madini katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni ofisa uendeshaji wa kampuni hiyo, Richard William na kushoto ni mmoja wa wawakilishi wa Serikali kwenye mazungumzo hayo, Profesa Florens Luoga. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Baada ya miezi sita tangu Serikali izuie usafirishaji wa makinikia na mazungumzo kati yake na kampuni hiyo kuanza, mwanga wa kuipata Tanzania mpya umeanza kujitokeza kutokana na maeneo tisa ya msingi kuridhiwa.

Dar es Salaam. Baada ya mazungumzo ya siku 80, kampuni ya Barrick Gold Mine imekubali yaishe na kuamua kutoa ‘kishika uchumba‘ cha Sh660 bilioni.

Baada ya miezi sita tangu Serikali izuie usafirishaji wa makinikia na mazungumzo kati yake na kampuni hiyo kuanza, mwanga wa kuipata Tanzania mpya umeanza kujitokeza kutokana na maeneo tisa ya msingi kuridhiwa.

Kwa pamoja, wajumbe wa pande mbili yaani Serikali na Barrick, jana waliwasilisha kwa Rais John Magufuli ripoti ya makubaliano yaliyoafikiwa kutoka kwenye mazungumzo yanayoendelea katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini hapa.

“Kwa makubaliano haya, sasa Barrick ni ndugu zetu. Huu ni mwanzo wa kuitengeneza Tanzania mpya hakuna mtu atakayekuja kututengenezea nchi yetu,” alisema Rais Magufuli.

Wawakilishi wa pande hizo wanaoendelea na mazungumzo ya kutafuta muafaka waliwasilisha ripoti ya mazungumzo yanayoendelea ambayo yamejikita kwenye maeneo matano. Tayari manne yamepata ufumbuzi isipokuwa faini ya Dola190 bilioni za Marekani ambayo inaendelea kujadiliwa.

Mwenyekiti wa wawakilishi wa Tanzania ambaye ni waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi aliyataja maeneo ya mjadala huo kuwa ni muundo na mfumo mpya wa uendeshaji wa kampuni za Barrick, kubadilisha uendeshaji wa madini na kuwanufaisha zaidi wananchi wanaoizunguka migodi.

Mengine ni kubadilisha mikataba ya madini (MDAs) ili iendane na sheria mpya zilizopo kwa lengo la kuongeza ushiriki na mapato ya Serikali pamoja na kuainisha fidia ya makosa ya kampuni tanzu za Barick. Wakati mengine manne yakiwa yamepata muafaka, la mwisho bado linajadiliwa.

Pia, waziri huyo aliyataja maeneo tisa ambayo mpaka sasa yamepata muafaka. Kwanza, alisema kampuni hiyo yenye asilimia 63.9 za hisa za Acacia inayoendesha migodi ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi imekubaliana na matakwa yote ya sheria mpya za madini.

Miongoni mwa mapendekezo ya sheria tatu za usimamizi wa rasilimali za Taifa zilizopitishwa kwenye Bunge la bajeti la mwaka huu ni kujengwa kwa mtambo wa kuchenjua dhahabu nchini, madini yote yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi kukaguliwa na kulipa ada ya ukaguzi ambayo ni sawa na asilimia moja ya thamani ya madini husika na Serikali kumiliki walau asilimia 16 ya hisa kwenye kila mgodi.

Profesa Kabudi alisema tayari masharti hayo yameingizwa kwenye mfumo wa fedha kwa ajili ya utekelezaji.

Eneo la pili alisema ni kuanza kugawana faida nusu kwa nusu. Itakumbukwa kwamba kabla ya utaratibu mpya kuanza migodi ilikuwa inalipa kodi ya kampuni ambayo hata hivyo taarifa zinaeleza kwa miongo miwili ya uchimbaji na uzalishaji, nyingi hazikulipa.

Makubaliano hayo ni tofauti na umiliki wa asilimia 16 ya hisa ambazo Serikali itakuwa inamiliki kwenye migodi ya kampuni hiyo.

Katika kufanikisha hilo, akaunti zote za benki pamoja na makao makuu ya Barrick yatamishiwa nchini. Serikali imependekeza makao makuu yahamishiwe Mwanza ingawa wanaweza kuwa na ofisi nyingine mkoa mwingine.

Katika mwelekeo huo mpya, itaanzishwa kampuni mpya ya uendeshaji wa migodi itakayoongozwa na Mtanzania ambako Serikali itakuwa na wawakilishi kwenye bodi ya wakurugenzi na kwenye kila mgodi.

Vilevile, sehemu kubwa ya kazi za mgodini zitafanywa na Watanzania pamoja na kuimarisha huduma za jamii kwenye maeneo yanayozunguka mgodi husika.

Katika kuimarisha ajira, kampuni hiyo imekubali kuachana na wafanyakazi wa mikataba badala yake itakuwa nao wa kudumu ambao hawatakaa kwenye makambi. Sambamba na hilo, Watanzania watapewa nafasi za juu za uongozi.

Sambamba na hayo, Barrick itajenga barabara kwenda Bulyanhulu ili kurahisisha usafiri wa wafanyakazi hao.

Eneo la sita ni kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha utafiti wa kujenga kiwanda cha kuchakata makinikia sambamba na maabara maalumu ya kuyapima. Kwa muda mrefu suala la ujenzi wa mtambo wa kuchenjua madini lilishindikana kutokana na sababu mbalimbali ikielezwa kwamba haliwezekani kutokana na gharama kubwa na Tanzania haina mchanga wa kutosha kukidhi mahitaji ya mitambo hiyo.

Eneo la saba lilikuwa mustakabali wa makinikia yatakayopatikana kuanzia sasa, baada ya makubaliano hayo. Waziri alisema madini mengine nje ya dhahabu, shaba na fedha yatakuwa ya Serikali.

Kamati zilizoundwa na Rais zilibaini uwapo wa madini mengine tofauti na yaliyomo kwenye mkataba ambayo yana thamani kibiashara. Madini hayo kuanzia sasa yatakuwa mali ya Serikali ambayo itaamua sehemu ya kuyauza.

Mabadiliko mengine yaliyofanywa ni kuzipa nguvu mahakama za ndani. Baada ya makubaliano hayo Rais alisema yatazingatiwa kwenye mikataba yote ya madini yanayochimbwa nchini mfano almasi na Tanzanite, kesi au mashauri yote yatatatuliwa kwa vyombo vya sheria vya ndani. Aidha, imekubalika wazawa watapewa kipaumbele katika kazi za ukandarasi zitakazohitajika kwenye migodi.

Wakati mazungumzo kuhusu faini kwa makosa mbalimbali yaliyofanywa na kampuni tanzu za Barrick, uongozi wake umeamua kulipa Dola300 milioni za Marekani (zaidi ya Sh660 bilioni).

“Majadiliano yalikuwa magumu mpaka kuupata muafaka huu,” alisema Profesa Kabudi.

Licha ya kutaka fedha hizo zilipwe haraka ili zifanye kazi nyingine nchini, Rais alisema makubaliano yaliyofikiwa ni ya aina yake barani Afrika na anaamini nchi nyingi zitakuja kujifunza.

“Tunayo miradi mingi kama vile Stigler’s gorge, reli na barabara. Nataka hizi fedha wazilipwe haraka kwa sababu ninazihitaji,” alisema Rais Magufuli.

Baada ya mazungumzo na Barrick, Rais aliwapongeza wajumbe wanane wanaoshiriki na kuwataka waendelee kufanya hivyo kwenye madini mengine.

“Ambaye hatataka mazungumzo aondoke, atuachie madini yetu. Tutafanya hivi kwenye madini yote,” alisisitiza huku akiahidi kuwatunuku wajumbe hao kwa vyeti maalumu kwa kuutambua mchango wao kwenye suala hili.

Kwa mara ya kwanza, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Barrick, Profesa John Thornton na mkurugenzi mtendaji wa Acacia, Brad Gordon wameongozana kuja kushiriki kikao hicho muhimu kwa mustakabali wa operesheni zao nchini.

Awali, Profesa Thornton alikuja nchini Juni kukutana na Rais Magufuli kuzungumzia zuio la usafirishaji wa makinikia kabla wataalamu wake hawajaja kutafuta muafaka wa suala hilo kwenye mazungumzo yanayoendelea.

Kati yao, ni mwenyekiti pekee aliyepata nafasi ya kuzungumza kwenye kikao cha jana. Akieleza maendeleo yaliyopatikana mpaka sasa, Profesa Thornton alisema muafaka uliopatikana utasaidia kuimarisha uhusiano uliopo kati ya kampuni hiyo na Serikali.

Kila kilichoridhiwa, mwenyekiti huyo alisema kitasubiri baraka za bodi ya wakurugenzi waliopo Uingereza msimamo uliowahi kutolewa na Acacia kabla mazungumzo hayo kuanza.

Kuhusu wazawa kuwa kwenye nafasi za uongozi pamoja na bodi za wakurugenzi, mwenyekiti huyo alisema: “Kwa makubaliano haya, kila upande utafahamu kinachoendelea na kuwa na imani na mwenzake.”

Utekelezaji wa makubaliano hayo yatakuwa mwendelezo wa uamuzi uliofanywa awali na Serikali kuzuia usafirishaji wa makinikia kiasi cha watendaji kadhaa waliokwenda kinyume na msimamo uliokuwa unapendekeza kutumbuliwa.

Licha ya watumishi, uliokuwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ulivunjwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuagizwa kuanza kuwachunguza watendaji wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kuliingiza Taifa kwenye hasara kwa muda mrefu.