Utouh: Msitumie madaraka kama mnaongoza familia zenu

Muktasari:

  • Autaja uongozi akiufananisha na taasisi inayopaswa kuheshimiwa, Nduga, Makinda wazungumza

Dodoma. Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema iko haja kwa wenye mamlaka kutengeneza nafasi zao zibaki kama taasisi na si kuzifanya kama mali ya familia.

Utouh alitoa kauli hiyo jana jijini hapa wakati akizungumza kwenye warsha ya asasi za kiraia (Azaki), ambako yeye na spika mstaafu, Anne Makinda walikuwa wasemaji kuhusu masuala ya uongozi.

Alisema kuna baadhi ya watu wameshindwa kutafsiri kuhusu dhana ya uongozi na badala yake wanachukua madaraka yanakuwa mali ya familia badala ya taasisi.

“Uongozi ni taasisi, tuepuke kufanya uongozi kuwa mali ya familia, hata kwenye urais msiruhusu aje mtu kufanya iwe ni mali ya familia wakati mnajua ni taasisi,” alisema Utouh ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya Wajibu.

Utouh alisema uongozi siku zote ni jalala hivyo lazima pawepo na kuvumiliana ili kukubaliana kwa masilahi ya nchi.

“Kingine msifanye kazi kwa mazoea, yaani mtu anaingia na kudumu miaka mitano yote hakuna anachofanya badala yake ni kuendeleza waliyofanya wenzake tu, kwa nini usiwaze yako na wewe? Halafu lazima mfanye uamuzi siyo mtu analetewa faili anadumu nalo hata hafanyi uamuzi mwisho anachelewesha mambo,” alisema.

Akichangia hoja ya Utouh, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema maoni ya mstaafu huyo ni sahihi lakini yamechelewa.

Alisema shida inayowapata viongozi ni woga. Alisema Utouh angeweza kutoa kauli hiyo akiwa bado madarakani lakini amesubiri hadi amestaafu.

“Si unaona hata NGO ambazo zilianzishwa na waliokuwa wake za marais baada ya waume zao kutoka zipo nyumbani, hicho ndichoo anachokataa mzee huyu (Utouh),” alisema Kibamba.

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alisema kauli ya Utouh ni sahihi lakini hajatofautisha kwa sababu mshahara ni mali ya familia ila madaraka ndiyo mtu aliyepewa.

Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamid Bobale alisema viongozi wengi wameshindwa kuiga nyayo za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye alifanya kila kitu kwa masilahi ya umma.

Bobale alisema kama Mwalimu angeamua kuiangalia familia yake, hata sasa wangekuwa juu zaidi na Butiama alikozaliwa ungekuwa mji wenye hadhi kubwa.

Katika mjadala huo, Utouh alikumbusha kuhusu ripoti yake ya mwaka 2012 iliyowang’oa mawaziri wanane akisema hajawahi kujutia, kwa sababu anaamini alisimamia vyema wajibu wake na ndiyo maana hata anapokutana nao wanasalimia vizuri.

Alisema kitendo hicho kiliwagusa wengi na hata kumwambia kuwa na tahadhari lakini hakujali kwa kwani hakuwa amemuonea mtu.

Alisema Watanzania wengi wanafanya kazi kama watu wenye matarajio ya kudumu milele bila ya kujua nafasi zao walizikuta na wataziacha, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa uangalifu mkubwa bila kuvunja sheria za nchi.

Bungeni ni kuvumiliana

Akizungumza katika warsha hiyo, Makinda ambaye alikuwa Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda akizungumza kwenye mjadala huo alisema siri ya uongozi ndani ya Bunge ni kuvumiliana na kupendana kama watu wamoja.

Alisema katika uongozi wake alilumbana na wabunge lakini mwisho wa yote walikula, kunywa na kucheza muziki pamoja.

Alikemea tabia ya baadhi ya wabunge kubeba siri za Bunge na kuzianika hadharani badala ya kuziacha bungeni.

Hata hivyo, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema kauli ya Makinda ni sahihi lakini anasahau kuwa Bunge lake lilikuwa tofauti na Bunge la sasa.

Kuhusu siri za Bunge, alisema kila kitu huwa kinajadiliwa kwenye kamati au vikao lakini kikifika bungeni siyo siri tena.

Imeandikwa na Habel Chidawali, Sharon Sauwa na Nazael Mkiramweni