VIDEO: Magufuli awaweka kikaangoni Ma RC, DC

Muktasari:

Rais  John Magufuli leo Jumatayun Oktoba 15, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na wakimbiza Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2018, Ikulu jijini Dar es Salaam na kuagiza wakuu wa mikoa na wilaya ambazo Mwenge wa Uhuru umebaini kasoro kujieleza

Dar es Salaam: Rais John Magufuli amewataka wakuu wa mikoa na wilaya zote ambazo zimekutwa na miradi yenye dosari wakati wa mbio za mwenge kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kutoa maelezo ndani ya siku 10 na kurekebisha dosari zilizojitokeza.

Pia, ameagiza wakuu wa mikoa na wilaya katika halmashauri tano ambazo zimefanya udanganyifu kwa miradi iliyotembelewa na mwenge mwaka jana kutoonekana mwaka huu, wajieleze kwa kina kabla ya kuchukuliwa hatua.

“Waziri Mkuu nataka yale maelezo ya kina watoe sasa, kwa nini wanadanganya mwenge, kwa nini wanamdanganya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni kiini na mwanzilishi halali wa mwenge” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Ikulu Dar es Salaam, alipofanya mazungumzo na wakimbiza Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2018 na kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Awali, Waziri Mkuu Majaliwa akitoa maelezo ya wakimbiza mwenge hao wakiongozwa na Charles Kabeho amesema wamekimbiza katika halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji 195 nchini.

Amesema tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu walikuwa wakifanya ukaguzi wa kina wa miradi ya maendeleo ili kubaini ubora na manufaa ya mradi husika kwa wananchi.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama amesema katika mbio hizo jumla ya miradi 1,432 yenye thamani ya Sh660.6 bilioni imezinduliwa, kufunguliwa na kuwekwa mawe ya msingi, huku miradi 80 iliyopo katika halmashauri 64 ikikutwa na dosari mbalimbali.

Mhagama amebainisha dosari hizo kuwa ni pamoja na ubora hafifu wa miradi na kukosekana kwa uhalisia wa thamani ya mradi na kwamba walikagua miradi 94 iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka jana na kubaini miradi mitano kati yake haifanyi kazi.