VIDEO: Mambo mawili aliyoyakosa Sugu akiwa gerezani

SUGU AWEKA HADHARANI MAMBO ALIYOKUWA AKIYAKUMBUKA KUHUSU BUNGE AKIWA GEREZANI

Muktasari:

Ni katika kipindi ambacho alikuwa akitumikia kifungo cha miezi mitato katika Gereza Kuu la Ruanda

Dodoma. Juzi Mei 21, 2018 mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu  aliingia bungeni kwa mara ya kwanza tangu aachiwe kwa msamaha wa Rais John Magufuli, Mei 10 mwaka huu.

Baada ya kurejea bungeni, wabunge wa upinzani walilipuka kwa furaha wakimshangilia huku wakigonga meza zao kwa takribani dakika mbili, hali iliyosimamisha shughuli za Bunge kwa muda.

Akizungumza na MCL Digital leo Mei 23, 2018 mbunge huyo ameweka wazi mambo mawili aliyoyakosa katika kipindi cha miezi sita ambacho hakushiriki vikao vya chombo hicho cha dola.

Sugu aliyeingia bungeni akiwa amevaa suti yenye nembo inayoonyesha namba ya mfungwa yenye taarifa za kifungo alichotumikia, ameyataja mambo hayo kuwa ni, kushindwa kuwawakilisha wananchi wa jimbo lake na Watanzania na kutokutana na marafiki na wabunge wenzake.

Sugu na Katibu wa Chadema, Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga walihukumiwa Februari 26, 2018 kwenda jela miezi mitano na Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mbeya baada ya kuwakuta na hatia ya kutoa lugha ya fedheha shidi ya Rais John Magufuli. Siku chache kabla ya kumaliza kifungo chao, waliachiwa huru kwa msamaha wa Rais.

 Uwakilishi wa wananchi 

“Jambo la kwanza na muhimu ambalo nilishindwa kulifanya nilipokuwa gerezani ni ile nafasi ya kuwawakilisha wana Mbeya na kutoa mchango na hoja mbalimbali ambazo ni kwa maslahi ya wana Mbeya na Taifa kwa ujumla,” amesema Sugu.

Kukosa fursa ya kukutana na marafiki

Jambo jingine alilolieleza Sugu ambaye pia ni msanii wa Hip Hop ni kutokutana na marafiki na wabunge wenzake.

“Nimekuwa mbunge kwa miaka minane. Unapokuwa hapa kwa muda huo unakuwa na marafiki, kwa hiyo niliwa-miss wabunge wa vyama vyote. Si unajua tunawashikaji hata upande wa pili (CCM), japo tunapokuja katika mambo ya kitaifa wanatukataa, lakini bado tuna mahusiano mazuri,” amesema Sugu.


Alichokifanya baada ya kuingia bungeni

Sugu pia anaikumbuka siku aliposhiriki kikao cha kwanza cha Bunge tangu atoke gerezani.

Amesema baada ya kushangiliwa na wabunge wenzake na kusalimiana nao alikwenda kuketi na kuanza kupitia baadhi ya nyaraka.

“Unajua nilifanya nini mara baada ya kufika katika kiti na kuketi? Nilipitia nyaraka chache zilizotolewa wakati nikiwa gerezani. Zilikuwa za wizara mbalimbali na ingawa zilitolewa wakati sipo ila ni vyema kuzipitia ili kuzielewa kwa maslahi yangu binafsi, Watanzania watu walionichagua,” amesema.