Viroba sasa vyaitwa subufa, samaki mkavu

Muktasari:

  • Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili wilayani hapa umebaini viroba vikiendelea kuuzwa kwa wateja wanaofahamika kwa kutumia majina hayo mapya.
  • Mmiliki wa baa (jina linahifadhiwa), alipoulizwa sababu za kuendelea kuuza vinywaji hivyo wakati vimepigwa marufuku, alisema wanafanya hivyo ili kupunguza hasara waliyopata kwa kuwa Serikali ilitangaza kuviondoa sokoni wakati wengine wamejaza kwenye maghala yao.

Vwawa. Baada ya Serikali kuzuia pombe kali zinazofungashwa kwenye mifuko ya plastiki maarufu viroba, baadhi ya wafanyabiashara wilayani Mbozi, mkoani Mbeya wamebuni njia mpya ya kuziuza kwa kutumia majina bandia yakiwamo subufa, samaki mkavu au maziwa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili wilayani hapa umebaini viroba vikiendelea kuuzwa kwa wateja wanaofahamika kwa kutumia majina hayo mapya.

Mmiliki wa baa (jina linahifadhiwa), alipoulizwa sababu za kuendelea kuuza vinywaji hivyo wakati vimepigwa marufuku, alisema wanafanya hivyo ili kupunguza hasara waliyopata kwa kuwa Serikali ilitangaza kuviondoa sokoni wakati wengine wamejaza kwenye maghala yao.

Mfanyabiashara huyo aliiomba Serikali iwaruhusu wamalizie akiba ya vinywaji hivyo waliyokuwa nayo ili kupunguza hasara.

Mteja aliyekuwa akinywa kinywaji hicho, Yohan Daudi mkazi wa Vwawa alisema analazimika kuvitafuta viroba kwa sababu alivizoea na vinauzwa bei nafuu ikilinganishwa na bia.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wilaya ya Mbozi, Yohana Mwajeka alipoulizwa kama anafahamu wafanyabiashara bado wanauza viroba, alisema ni kweli na kwamba wapo katika mazungumzo na Serikali ili iongeze muda wa kumalizia viroba vyote kwenye maghala.

“Hivi sasa wadhibiti uzalishaji, lakini wafanyabiashara walionunua vingi wanaomba wamalizie mzigo,’’ alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema ataagiza polisi wafanye msako kuwabaini wanaoendelea kuuza viroba kwa mbinu zozote zile.

Alisema Serikali ilishatoa maelekezo na kwamba ni marufuku kwa mfanyabiashara yeyote kuendelea kuuza viroba na kuwataka wananchi wote kuheshimu amri hiyo halali.