Vyama vya siasa vyatishwa

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema chama cha siasa kitakachokiuka taratibu na sheria kitajifuta chenyewe kwa kukosa sifa.

Muktasari:

  • Jaji Mutungi ametoa kauli hiyo baada ya kutafutwa na gazeti la mwananchi kutoa ufafanuzi wa kile kilichodaiwa kuwa ana njama ya kutaka kuifutia usajili Chadema.
  • Juzi, Baraza la Wazee wa Chadema lilisema kuna njama za kukifuta chama hicho zinazopangwa kupitia ofisi ya msajili huyo.

Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema chama cha siasa kitakachokiuka taratibu na sheria kitajifuta chenyewe kwa kukosa sifa.

Jaji Mutungi ametoa kauli hiyo baada ya kutafutwa na gazeti la mwananchi kutoa ufafanuzi wa kile kilichodaiwa kuwa ana njama ya kutaka kuifutia usajili Chadema.

Juzi, Baraza la Wazee wa Chadema lilisema kuna njama za kukifuta chama hicho zinazopangwa kupitia ofisi ya msajili huyo.

Baraza hilo pia lilimtupia lawama Jaji Mutungi kuwa anafanya hivyo kwa kutimiza matakwa ya watawala kwa kutumia mwamvuli wa Baraza la Vyama vya Siasa.

Kauli ya wazee hao ilitolewa kwa kurejea matukio kadhaa yakiwamo ya kuahirishwa kwa vikao vya Agosti 29 na 30 na Septemba 3 na 4, vilivyopangwa kufanyika kati yao na msajili huyo.

Walidai vikao hivyo vilipangwa kufanyika karibu na Septemba Mosi ambayo Chadema ilipanga kufanya maandamano ya Ukuta nchi nzima, lakini viliahirishwa bila kupewa taarifa ya maandishi.

Wasiwasi huo wa Chadema kufutwa katika orodha ya vyama vya siasa nchini, ulianza kuvuma baada ya ofisi ya msajili kusema itaanza kufanya uhakiki wa vyama hivyo nchini.

Hata hivyo, alipozungumza na gazeti hili jana kuhusu tuhuma hizo, Jaji Mutungi alisema wazee wa baraza hilo wana haki ya kufikiria hivyo lakini hakuna kitu kama hicho. “Vyama vya siasa vitajifuta vyenyewe kwa kukiuka sheria na taratibu zinazofanya viendelee kuwapo,” alisema.

Jaji Mutungi alitoa rai kwa wanasiasa kuepuka kuendesha vyama vyao kwa hisia.

 Alisema uhakiki huo unalenga kupima na kujiridhisha kama vyama vilivyosajiliwa vinafuata taratibu za usajili.

“Siwezi kusajili vyama vipya wakati hata hivi nilivyonavyo sijavihakiki,” alisema.

Alifafanua kuwa uhakiki wa vyama hufanywa kila baada ya mwaka mmoja au miezi sita.

Alisema uhakiki huo utaanza baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi za Hesabu za Serikali (CAG).