Wabunge Zanu PF wamvuruga Rais Mnangagwa

Muktasari:

Ripoti ambazo gazeti la The Standard lilipata mwishoni mwa wiki zinasema wabunge wengi wa Zanu PF wanataka uchaguzi uahirishwe walau kwa miaka mitatu.

Harare, Zimbabwe. Rais Emmerson Mnangagwa anakabiliwa na mvutano wa ndani juu ya uchaguzi wa mapema baada ya wito wake wa kutaka ufanyike Agosti kama ilivyopangwa kupingwa na baadhi ya wabunge wa chama chake cha Zanu PF.

Ripoti ambazo gazeti la The Standard lilipata mwishoni mwa wiki zinasema wabunge wengi wa Zanu PF wanataka uchaguzi uahirishwe walau kwa miaka mitatu.

Wabunge hao imeelezwa wameanza kufikiria kulitumia Bunge lifanyie marekebisho Katiba ili uchaguzi huo uliopangwa ufanyike miezi mitano ijayo uahirishwe.

Wabunge wa Zanu PF imeelezwa wana hofu ya kushindwa vibaya viti vyao kwa wanajeshi ambao wamepewa nafasi ya kugombea ubunge katika uchaguzi ujao kupitia tiketi ya Zanu PF.

Hii imeelezwa kwamba ni hatua ya kuwapa zawadi wamajeshi kwa kufanikisha operesheni iliyowezesha kumpoka mamlaka Robert Mugabe na kumpa Mnangagwa. Wabunge wa Zanu PF ambao wamekuwa kwenye migawanyiko ya muda mrefu pia wana hofu kwamba chama bado kinakabiliwa na vurugu na mkanganyiko na wanaweza kupoteza viti kwa wagombea wa upinzani wa MDC-T ambao pia wana migogoro ikiwa uchaguzi utaendelea kama ratiba ilivyopangwa.

Vyanzo vya uhakika vililiambia The Standard kwamba wakati Mnangagwa anahaha kuandaa uchaguzi mwaka huu ili kuhalalisha utawala wake, wabunge wake wanampinga na wanaomba msaada kwa MDC-T MPs watumie Bunge kuahirisha uchaguzi.

Habari zinasema MDC-T wamevutiwa na wazo hilo kwani nao walikuwa wanapendekeza uchaguzi uahirishwe ili kumpa kiongozi wao Morgan Tsvangirai muda wa kutosha kupata ahueni kutokana na maradhi ya kansa yanayomsumbua.