Wabunge wataka ‘road license’ ifutwe

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji

Muktasari:

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikiendelea kuwaweka kwenye kumbukumbu za wasiolipa ‘road licence’ wenye magari yaliyoegeshwa kutokana na ubovu au ajali.

Dodoma. Serikali imeahidi kuifanyia marekebisho sheria inayoagiza tozo ya umiliki wa vyombo vya moto (road license) ili kuondoa kero kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amesema hayo bungeni leo (Ijumaa) alipojibu swali la Dk Raphael Chegeni aliyetoa pendekezo hilo ili kodi hiyo iendane na matumizi halisi ya vyombo vya moto barabarani.

"Tozo hii ipo kisheria. Serikali imesikia mapendekezo ya wabunge na itaangalia namna nzuri ya kuboresha ukusanyaji wa mapato hayo," amesema Dk Kijaji.

Wabunge wengi, akiwamo Spika wa Bunge Job Ndugai wamependekeza kufutwa kwa kodi hiyo inayowaathiri zaidi walioegesha magari kwa muda mrefu kutokana na ubovu au ajali.