Wabunifu wa Tehama wapigiwa debe


Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), imezitaka taasisi za fedha nchini kuziona fursa zilizopo kwa wabunifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na kuwawezesha mitaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Costech, Dk Hassan Mshinda alisema hayo alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari.

Alisema taasisi za fedha zimejielekeza zaidi kwenye miradi ya bidhaa au huduma zinazoonekana na kuisahau sekta hiyo ndogo inayokua kwa kasi.

“Watu wa benki hawaelewi chochote kuhusu ubunifu unaofanywa huku, hivyo kutoziona fursa zilizopo. Wabunifu hawa wana mawazo yanayoweza kutoa matajiri endapo watawezeshwa kwa mitaji midogo wanayoihitaji kwa kianzio,” alisema Dk Mshinda. 

Kituo cha Bun Hub kilichopo Costech kinatoa fursa kwa wabunifu wa programu zinazotatua kero mbalimbali zilizopo kwenye jamii kwa kutumia Tehama.

Ndani ya miaka mitano iliyopita, zaidi ya vijana 5,000 wamewezeshwa, kampuni 300 za kibunifu zimeanzishwa, miradi 68 imetekelezwa na zaidi ya wanafunzi 450 wa vyuo vikuu wamepewa mafunzo ya vitendo.

Mwanzilishi wa Bun Hub, Jumanne Mtambalike alisema endapo eneo hilo litatazamwa vizuri na wadau wakalipa kipaumbele, Tanzania itakuwa na mabilionea wengi baada ya muda mfupi.

“Kampuni za kibunifu ni biashara kubwa inayohitaji umakini kuisimamia. Vijana waliopo huku wana mtazamo wa mbali wanapoandaa programu zao zinazoweza kutumika kimataifa. Wanahitaji kushikwa mkono wanapoanza,” alisema Mtambalike ambaye ni mkurugenzi wa Kampuni ya Sahara Ventures.