Wachezaji Simba wamlilia Mo Dewji

Muktasari:

MO amekuwa akiidhamini Simba kwa muda mrefu na sasa anakaribia kununua hisa asilimia 49 za umiliki wa klabu hiyo, ametekwa leo asubuhi na watu wasiojulikana


Dar es Salaam. Wachezaji na wasanii mbalimbali wameonekana kuguswa na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu na mfadhili wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji 'Mo'.

Mo alitekwa leo Alhamis asubuhi Oktoba 11, 2018 wakati akiwa kwenye Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazoezi kwenye gym.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa  alisema Mo alitekwa na Wazungu wawili.

Wachezaji wa Simba na wasanii wameposti katika mitandao ya kijamii wakimtakia usalama tajiri huyo kijana Afrika.

Kipa namba moja wa wekundu hao wa Msimbazi, Aishi Manula ameandika, “Ewe mola wetu (Allah) mfanyie wepesi Mo Dewji kwenye mapito na mtihani alioupata, mfanye awe mwenye kuyashinda mapito hayo na kuwa huru.”

Kiungo wa timu hiyo, Shiza Kichuya amesema, “Mungu akulinde uwe salama, Amen  Mo Dewji.”

Nahodha wa mabingwa wao wa 2017/18, John Bocco yeye amesema, “Mungu akusimamie na kukulinda huko ulipo Inshaallah...atakuepusha na changamoto zote na kurudi salama.”

Beki wa wekundu hao wa Msimbazi, Shomary Kapombe amesema, “Ee Mungu nenda ukamtie nguvu na kumlinda na awe katika ushindi kwenye hili Mo Dewji tunakuombea na Mungu atakufanyia wepesi.”

Naye Mussa Mgosi amesema, “Vilio vya wana Simba, Yarabi tunakuomba habari yoyote ikija isiwe mbaya na nyoyo zetu Yarabi unazishuhudia zinavyopata maumivu, mpe ujasiri na nguvu ya kumponya katika hili Inshaallah, Mungu atamfanyia wepesi.”

Mshambuliaji wa kimataifa Meddie Kagere kupitia ukurasa wake wa Instagram Officialmeddiekagere amendika, “Mwenyezi Mungu akuepushe na hatari zote urejee salama Boss @moodewji????

Emmanuel Okwi ameandika, “Kila kitu kitakuwa sawa Mo Dewji.”

Miongoni mwa wasanii walioguswa na tukio la Mo ni Jacquline Wolper aliyesema, “Mwenyezi Mungu akawe ngao yako baba, binadam si kitu chini ya jua, jemedari ni mmoja tuu hakuna mwenye vitisho wala mamlaka kumzidi yeye. Tupo nyuma yako.”

Steve Nyerere amesema pole familia, najua na kutambua kila mtu sasa hivi anaongea lake, cha muhimu ni kuwapa ushirikiano jeshi letu la polisi.

“Kaka yetu, rafiki yetu apatikane. Jambo kama hili halina ushabiki wa Simba wala Yanga wote tunaungana kumuombea Mo Dewji apatikane akiwa salama. Mungu ibariki Tanzania. Amina.”