Wachimbaji wadogo waiangukia Serikali

Muuzaji mdogo wa madini ya kopa, Mohamed Mkwayu akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu zuio la kusafirisha nje ya nchi mchanga wa dhahabu lililotolewa na Rais John Magufuli. Picha na Ericky Boniphace.

Muktasari:

Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana, wachimbaji hao walisema kutokana na zuio hilo wanapata hasara ya kutunza makontena yaliyokuwa na mchanga wenye madini ya kopa na metaliki na hasara ya kusimamisha mgodi usifanye kazi.

Dar es Salaam. Wachimbaji wadogo wa madini kutoka maeneo mbalimbali nchini wameiomba Serikali kuondoa zuio la kusafirisha kontena za mchanga nje ya nchi.

Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana, wachimbaji hao walisema kutokana na zuio hilo wanapata hasara ya kutunza makontena yaliyokuwa na mchanga wenye madini ya kopa na metaliki na hasara ya kusimamisha mgodi usifanye kazi.

Mwenyekiti wa wachimbaji hao, Thobias Rweyemamu alisema jumla ya kontena 60 zenye madini ya kopa na shaba zenye madini ya nickel zimekwama kusafirishwa kutokana na zuio hilo la rais.

Malalamiko ya wachimbaji hao wadogo yamekuja baada ya Rais John Magufuli kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini nje ya nchi badala yake ametaka mchanga wote uchenjuliwe hapa hapa nchini.

Mwenyekiti wa wachimbaji hao alisema kuwa hasara wanayopata ni pamoja na fedha ya kuhifadhia makontena hayo kwenye maghala ambapo kila siku kwa kontena moja hulipa dola 20 ambayo ni sawa na Sh 44,000.

Alisema mbali na gharama hiyo pia hupata hasara ya kulipia mgodi usiofanya kazi ambao kwa siku moja hugharimu Sh4 milioni kwa ajili ya malipo ya wafanyakazi, ulinzi wa mitambo na vifaa.

“Tupo hapa kumuomba Rais aondoe zuio hilo kwa sisi wachimbaji wadogo, inavyoonekana hakutulenga sisi aliwalenga wachimbaji wakubwa wa madini ya dhahabu, sisi huku hata hiyo kopa inapatikana kidogo sana, ”alisema Rweyemamu.

Naye Mohamed Mkwayu mchimbaji kutoka Mpwapwa alisema kwenye kopa hakuna dhahabu na inapokwenda kuchenjuliwa kinachokutwa ni dhahabu kidogo.

Alimuomba Rais aliangalie suala hilo kwa sababu wachimbaji wakubwa wa dhahabu wanaendelea na kazi zao kutokana na kuwa na mitaji mikubwa.

“Tuna familia, tumekopa fedha kwa ajili ya uchimbaji, zuio hilo linatufanya tushindwe kulipa madeni, kuhudumia familia, rais atuangalie na wahusika wasituchanganye na wachimbaji wakubwa, ”alisema Mkwayu.

Kwa upande wa Paulo Kalyembe alisema kuwa mchanga wanaochimba wao wa kopa hauna chembe ya madini ya dhahabu, hivyo kuunganishwa katika zuio hilo ni kuwaonea.