Wachina kujenga Dubai ndogo ya Tanzania Ubungo

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage

Muktasari:

  • Nchi hizo zimekuwa zikibadilishana wataalamu, uzoefu, biashara na miradi mbalimbali.

Dar es Salaam. China inakusudia kujenga Kituo cha Kisasa cha Kibiashara katika eneo la Ubungo, kikiwa na uwezo wa kukusanya shughuli zote za biashara na mahitaji ya nyumbani.

Kituo ambacho kitakapokamilika kitalifanya Jiji la Dar es Salaam lifahamike kama ‘Dubai ndogo ya Tanzania’.

Pia, kituo hicho ambacho ujenzi wake unatarajiwa kuanza mwaka huu na kukamilika baada ya miezi 15, kinatajwa kuwa tofauti na Soko Kuu la Kariakoo, kitakuwa na zaidi ya maduka 3,000, maghala madogo zaidi 300 na eneo lenye uwezo wa kuhifadhi magari 5,000. Kitajengwa na Kampuni ya LingHang na kusimamiwa na Serikali ya China.

Alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema wanaolifahamu vizuri ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Hata hivyo, Ofisa Habari wa TIC, Upendo Gondwe alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kampuni ya LingHang, kituo hicho kimepangwa kujengwa kandokando ya eneo kinakoishia  mabasi yaendeayo haraka (BRT), kitakuwa na maeneo ya kibiashara kama benki, ofisi, maduka makubwa na muonekano wake umeelezwa utakuwa wa kuvutia.

“Kukamilika kwa kituo hicho cha kipekee katika eneo la Afrika Mashariki, kutafungua ukurasa mpya kwa wafanyabiashara wa ndani na nje kwa sababu sasa wataweza kufanya shughuli zake katika mazingira mazuri na rafiki,” inasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na LingHang.

Inaelezwa wastani wa ajira 20,000 zinatarajiwa kuzalishwa na kituo hicho, huku kikitarajia kuchangia biashara ya usafirishaji nje na ndani kwa asilimia 30.

 Ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya makubaliano yaliyotiwa saini Julai 28, 2016 nchini China kati ya nchi hizo mbili.

Tanzania na China zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia kwa miaka mingi na hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kwanza barani Afrika, Rais Xi Jinping alianzia Tanzania.