Wadaiwa sugu kukatiwa maji

Meneja Uhusiano wa Dawasco, Everlasting Lyaro.

Muktasari:

Dawasco imewatangazia wateja wake kwamba atakayebainika kuwa na deni na kukatiwa maji atalazimika kulipa faini ys Sh 30,000

Shirika la Majisafi na Majitaka (Dawasco), limesema wadaiwa sugu wa maji watasitishiwa huduma hiyo kuanzia leo.

Meneja Uhusiano wa Dawasco, Everlasting Lyaro amesema mchakato huo wa kusitisha huduma itahusisha mkoa wa Dar es Salaam, Miji ya Kibaha na Bagamoyo.

Amesema hatua hiyo itawahusu wateja wenye madeni ya ankara ya maji kuanzia mwezi mmoja  na kuendelea, wateja waliofanya malipo ya nusu (part payment) katika Ankara  zao za maji mwezi na wenye madeni sugu.

“Kumbuka ukisitishiwa huduma, gharama ya kurudisha ni Sh 30,000 lipa ili kuepuka usumbufu,”amesema Lyaro.

Lyaro amewataka wateja wa Dawasco kulipia ankara zao za huduma ya majisafi pamoja na madeni ya kipindi cha nyuma mapema ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma.