Wahandisi wa maji waonywa

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge

Muktasari:

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), Dk Zainab Chaula wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Malipo kwa Matokeo (Payment by Result) uliozinduliwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge mjini hapa.

Dodoma. Wahandisi wa maji nchini wametakiwa kujitathmini iwapo wanatosha kufanya kazi hiyo, ikiwa ni ngumu kwao waachie ngazi ili kupisha wengine.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), Dk Zainab Chaula wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Malipo kwa Matokeo (Payment by Result) uliozinduliwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge mjini hapa.

Dk Chaula alisema wapo baadhi ya wahandisi wamekuwa wakiishi kwa ujanja bila ya kujishughulisha na matatizo ya wananchi.

Alisema Tamisemi imeamua kuwafanyia tathmini wahandisi wa maji nchini na mojawapo ya kipimo ni upelekaji wa taarifa, zinazotakiwa wizarani kati ya tarehe 7 na 14 kila mwezi.

“Siamini na sielewi kwa nini mniambie mmeshindwa, nani anashindwa na kwa nini mwingine aweze, sihitaji kusikia nimefikia asilimia fulani... kila mmoja afikie lengo lake,” alisisitiza Dk Chaula.

Akizindua mpango huo, Waziri Lwenge (Pichani) alisema kuna mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya maji vijijini, lakini akawataka baadhi ya watendaji wabadilike na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Waziri Lwenge alisema mradi huo umejikita vijijini ambako tayari unatekelezwa kwenye halmashauri 179 kati ya 185.

Mwakilishi wa kutoka Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Thomas Alan alisema lengo la kusaidia miradi hiyo ni kutokana na umuhimu wake hasa matatizo ya maji kwa wananchi wa vijijini.

Alan alisema Serikali ya Uingereza itaendelea kufadhili miradi ya majisafi na salama kwa maeneo yenye shida ya huduma hiyo, hivyo alitaka itunzwe na kuendelezwa ikiwamo kuvifanyia ukarabati vituo ambavyo vimejengwa.