Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngoma bado ngumu kuinasua Mv Clarias majini

Mwonekano wa meli ya Mv Clarias ikiwa imepinduka katika Bandari ya Mwanza Kaskazini. Meli hiyo inayotoa huduma kati ya mwalo wa Kirumba na kisiwa cha Goziba wilayani Muleba mkoani Kagera, ina uwezo wa kubeba abiria 290 na tani 10 za mizigo. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Ofisa Mawasiliano wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Abdurahman Salim amesema dalili za kufanikiwa kuinasua meli hiyo iliyozama tangu Mei 19, 2024 zinaonekana.

Mwanza. Jitihada za kuinasua meli ya Mv Clarias zinaendelea ikiwa ni siku ya tatu tangu ipinduke Mei 19, 2024 ikiwa imeegeshwa katika bandari ya Mwanza Kaskazini bila kuwa na abiria wala mizigo.

Meli ya Mv Clarias inayofanya safari zake ndani ya Ziwa Victoria, ikitoa huduma mara mbili kwa wiki kati ya Mwanza na kisiwa cha Goziba, Muleba mkoani Kagera ina uwezo wa kubeba abiria 290 na tani 10 za mizigo.

Mmoja wa wahusika wanaonasua meli hiyo (jina limehifadhiwa) ameiambia Mwananchi Digital leo Jumanne Mei 21, 2024 kuwa tayari mbinu kadhaa za kuinasua meli hiyo majini zimeshafanyika bila mafanikio.

Amesema kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Mwanza pamoja na wadau mbalimbali wenye vifaa vya uokozi ikiwemo winchi, wamejaribu kuinasua meli hiyo inayoonekana upande wa nahodha kuegama kwenye tope bado hazijazaa matunda.

“Jitihada mbalimbali zimefanyika ikiwemo usaidizi wa kufunga minyororo kuja kwenye winchi na mitambo yenye nguvu ikiwemo tingatinga kunyanyua, lakini jitihada hizo zinafeli kutokana na uzito wa chombo chenyewe lakini pia kwa kuwa kiliegama kwenye matope hususani upande wa kichwa anapokaa nahodha, ndiyo sababu nyingine inayokwamisha kazi hiyo,”amesema ofisa huyo.

Hata hivyo, Ofisa Mawasiliano wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Abdurahman Salim amesema jitihada za kuitoa ndani ya maji meli hiyo zinaendelea na dalili za kufanikiwa kuinasua zinaonekana.

Amedai tayari wamefanikiwa kuisogeza pembeni kuruhusu meli nyingine ya MV Butiama inayofanya safari kati ya Halmashauri ya jijini la Mwanza na Wilaya ya Ukerewe kutoa huduma.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Kamila Laban amesema vikosi vya uokoaji viko eneo la tukio kutoa usaidizi wa kuinasua meli hiyo tangu siku ya kwanza.

“Askari wetu wa Zimamoto na Uokoaji wako pale kuhakikisha meli hiyo inatoka kwenye maji, wapo tangu siku ya kwanza wanalala huko kuhakikisha wanasaidia kwenda kufunga kamba, nyaya na shughuli zingine zinazohitaji kuzama ndani ya maji na wanaendelea na shughuli hiyo  kwa ajili ya kuiopoa na naamini Mungu akisaidia itatolewa majini," amesema kamanda huyo ambaye hata hivyo hakusema lini wanaweza kufanikiwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu Shirika la Uwakala wa Meli nchini (Tasac), Mohamed Salum tayari mtaalamu mbobezi wa masuala ya uundaji wa meli na mhandisi mtaalamu wa mitambo ya meli wamewasili jijini Mwanza kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.


Safari za Mv Butiama bado

Mwananchi Digital ilishuhudia baadhi ya abiria wanaofanya safari kati ya Mwanza mjini na Ukerewe wakiulizia tiketi za safari hata hivyo, wahudumu waliwajibu huduma zitarejea kesho Mei 22, 2024.

Mmoja wa abiria, Magreth Jafari ameiomba Serikali kuongeza juhudi ya kunasua meli ya Mv Clarias kuruhusu huduma za meli ya Mv Butiama kuendelea.

“Hii meli inarahisisha usafiri sana hasa kwa wafanyabiashara ambao wanaenda Ukerewe na kurudi Mwanza siku hiyohiyo kwa sababu ndani ya masaa mawili tu mtu unafika Ukerewe unafanya mambo yako saa nane mchana unageuza nayo kurudi Mwanza,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu kuanza kwa safari za Mv Butiama, Salim amesema kutokana na jitihada zinazoendelea kufanyika, safari hizo zinaweza kurejea kesho Jumatano Mei 22, 2024.

Tofauti kati ya kuzama na kupinduka

Baada ya tukio la meli hiyo kupinduka ikiwa imeegeshwa katika eneo lake lililopo Bandari ya Mwanza Kaskazini, baadhi ya wananchi wamekuwa wakijiuliza tofauti ya neno kuzama na kupinduka.

Akizungumzia tofauti ya maneno hayo, Nahodha wa Kivuko cha Nyehunge kinachofanya safari kati ya Mwanza mjini na Ukerewe, Manase Nkomola amesema kuzama ni kutitia kwa chombo kwenda chini kwa sababu za hitilafu za kiufundi au hali ya hewa, huku kupinduka ni chombo cha maji kulala ubavu au kulalia upande.

“Kuzama ni chombo ambacho kinashuka chini moja kwa moja  yaani inashuka nzima nzima inatitia chini ya maji lakini kupinduka kama ulivyopata taarifa ya Mv clarias ile ina maana imelala ubavu, hii imepinduka,”amesema