Wakulima wa pamba wabadili matumizi dawa ya kuua wadudu

Muktasari:

Serikali yaombwa kuwachukulia hatua za kisheria wakulima wote wanaotumia dawa hizo kinyume na matumizi

Kahama. Baadhi ya wakulima wa pamba wilayani hapa mkoani Shinyanga wamedaiwa kubadilisha matumizi ya dawa ya kuua wadudu kwenye zao hilo na kuitumia katika mahindi na nyanya.

Hali hiyo ilielezwa na ofisa kilimo kutoka Kampuni ya Nida Textile Mill (T) Limited, Issa Hamis ambaye alisema hali hiyo inadidimiza kilimo cha pamba licha ya Serikali kuweka utaratibu wa wakulima hao kupata dawa ya kumwagilia kwenye pamba.

“Dawa ya duduba ukimwagilia katika mahindi yanastawi vizuri sana na unaweza ukapata mavuno mengi, na ndiyo sababu ya wakulima wa pamba kutumia dawa hizi katika mazao ya mahindi na nyanya badala ya zao la pamba,” alisema.

Mkulima wa zao hilo kutoka Mbogwe, John Msha alisema ni kweli wakulima wamekuwa wakitumia dawa hizo katika matumizi ambayo si halali.

Msha alisema Serikali inatakiwa kuwachukulia hatua za kisheria wakulima wote wanaotumia dawa hizo kinyume na matumizi yake.

Meneja wa Kampuni ya Nida Textile Mill (T), Edison Peter alisema kwa mwaka huu wakulima wamelima pamba kwa wingi ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Alisema viwanda vingi vitaweza kuajiri wafanyakazi wa kuchambua pamba hasa msimu wa ununuzi utakapoanza Mei mwaka huu.

Hata hivyo, aliwataka wakulima kuacha tabia ya kumwagilia zao hilo mchana wa jua kali badala yake wafanye hivyo kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa nne asubuhi.

Pia, alisema wanaweza kumwagilia saa 11 jioni hadi saa moja jioni.